MWAKYEMBE AIPONGEZA KINONDONI KWA KUFANYA VIZURI KATIKA SEKTA YA MICHEZO
Posted On: October 2nd, 2019
Waziri Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe Harrison Mwakyembe ametoa pongezi hizo leo alipotembelea Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa lengo la kuwapongeza na kuwatia hamasa viongozi wanaofanya kazi iliyotukuka katika kukuza michezo nchini.
Mhe Mwakyembe ameyataja maeneo ambayo Kinondoni kupitia Timu yake ya mpira wa miguu KMC imefanya vizuri kuwa ni pamoja na Kupanda ligi kutoka daraja la kwanza na kumaliza ligi kuu ikiwa nafasi ya nne msimu uliopita.
Amepongeza mipango ya kujenga uwanja wa kisasa wa soka katika eneo la Mwenge, Kuanzisha Academy ya kulea vipaji vya soka kwa watoto na kuwa na Jezi bora kabisa ambapo KMC imekuwa timu inayoogopwa nchini.
Aidha ameahidi kuwa Wizara yake itakuwa bega kwa bega na Manispaa ya Kinondoni katika kuhakikisha mipango waliyojiwekea ya kuhakikisha Soka linaenda mbele zaidi inafanikiwa.
Awali akitoa taarifa mbele ya Mhe Waziri, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe Benjamin Sitta amesema uwanja unaotarajiwa kujengwa katika eneo la mwenge utatumika kama uwanja wa nyumbani kwa timu ya KMC, kutakuwa na hostel za vijana wa Academy na pia kutakuwa na fremu kwaaajili ya biashara nyingine.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment