KINONDONI KUVITAMBUA, KUVISAJILI NA KUVISIMAMIA VITUO 444 VYA BODABODA NA BAJAJI KATIKA MAENEO YAO Posted On: November 15th, 2018 Manispaa ya Kinondoni imedhamiria kuboresha chanzo cha mapato kitokanacho na vituo vya bodaboda na bajaji kwa kuhakikisha inavitambua, inavisajili na kuvisimamia vituo takribani 444, vilivyopo katika Kata na Mitaa ya Manispaa hiyo kwa kuzingatia,miongozo sheria, kanuni na taratibu zinazoelekeza kufanya hivyo. Akitoa muongozo wa zoezi zima la utambuzi huo, katika mkutano wake na madereva wa bodaboda na bajaji uliofanyika katika ukumbi wa King Solomon leo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh.Daniel Chongolo amesema, kwa kushirikiana na wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA kwa Manispaa ya Kinondoni, wanatakiwa kuhakikisha suala hilo la utambuzi linafanyika kwa umakini,na wakati, ikiwa ni pamoja na kusimamia tozo zao zitakazokuwa zikitolewa kwa mujibu wa sheria. "Manispaa ya Kinondoni, TARURA, itisheni kikao cha Uongozi wa Wilaya, kaeni nao, kubalianeni taratibu nzuri za kuendesha vikundi vyao, vitambueni, visajilini, na mvisimamie tozo zao."Amesisitiza Chongolo. Awali akitoa taarifa ya vituo hivyo vya bodaboda na bajaji, Mwenyekiti wao ndugu Festo Swai, amesema upo umoja wao uitwao CMPD, ulionzishwa kwa lengo la kusaidiana na kushughulikia changamoto zinazowakabili wao kama vikundi vidogo vidogo, zikiwemo kutosajiliwa na kutambuliwa, kutopatiwa mikopo ya vijana, kutozijua haki zao pindi wanapokutwa na kosa la barabarani, kuuwawa na kuporwa mali zao, pamoja na kupatiwa njia ya kusafirisha abiria mjini. Akijibu swali linalomtaka bodaboda au bajaji kupelekwa mahabusu pindi afanyapo kosa kwa niaba ya OCD Kinondoni, Inspekta Serengeti amesema, dereva wa bajaji au bodaboda kufanya kazi zake bila kuwa na leseni na viambata vyote atakiwavyo kuwanavyo dereva , atashitakiwa kwa kosa la usalama barabarani. Naye Afisa Maendeleo ya Jamii anayehusika na Mikopo, Bi Florah Msilu, katika kufafanua suala la mikopo kwa vijana amesema, kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Kinondoni imetenga takribani bilioni 2.7, kwa ajili ya mikopo, na kuwataka vijana wenye umri kuanzia miaka 18-35, katika vikundi kuchangamkia fursa hiyo. Huu ni Mkutano wa kwanza wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kukutana na madereva wa bodaboda na bajaji, pamoja na viongozi wao na kufanya nao mazungumzo ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero na changamoto walizonazo. Imeandaliwa na Kitengo cha Uhusiano na habari. Manispaa ya Kinondoni. KINONDONI KUVITAMBUA, KUVISAJILI NA KUVISIMAMIA VITUO 444 VYA BODABODA NA BAJAJI KATIKA MAENEO YAO Posted On: November 15th, 2018 Manis... + Read more »