WITO WATOLEWA KWA WANANCHI WAISHIO NA WATU WENYE ULEMAVU WILAYA YA KINONDONI Posted On: September 12th, 2018 KUHAKIKISHA WANASHIRIKIANA NA NIDA WILAYANI HAPO, KUWASAJILI KATIKA DAFTARI LA TAIFA NA KUWATAMBUA KWA LENGO LA KUPATIWA VITAMBULISHO VYA TAIFA. Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Daniel Chongolo, alipokuwa mgeni rasmi kwenye zoezi la usajili na utambuzi wa watu wenye ulemavu kwenye daftari la Taifa, lililofanywa na NIDA, kwa kushirikiana na SHIVYAWATA, pamoja na Ofisi ya Ustawi wa Jamii Manispaa ya Kinondoni, kwa lengo la kupatiwa vitambulisho vya Taifa. Amesema zoezi hili ni zuri, kwani kwa kufanya hivi ni kutekeleza haki ya msingi kikatiba na pia ni kutoa fursa ya watu wenye ulemavu kusajiliwa na kupatiwa vitambulisho vya Taifa, na kuwataka wananchi wanaoishi nao majumbani, kuhakikisha wanawaleta kwa ajili ya zoezi hilo la siku tatu la utambuzi na uandikishaji linaloendelea katika shule ya Ndugumbi Manispaa ya Kinondoni. "Wito wangu kwa wanakinondoni, wito wangu kwa wale wanaoishi na watu wenye ulemavu, naomba sana ndani ya siku tatu hizi, muwashawishi, wawalete, wawape fursa watu wenye ulemavu kutumia haki yao ya msingi waliyopewa ya kujisajili kwenye daftari la Taifa, kwa ajili ya kupata vitambulisho vya Taifa".Amesisitiza Chongolo. Awali akitoa taarifa ya zoezi hilo, Afisa Msajili wa NIDA Wilaya ya Kinondoni Ndg. Dickson Mmbaga amesema, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Kinondoni kupitia zoezi hili tumetambua, tumesajili, tumeweka mazingira wezeshi na kupata takwimu zitakazosaidia kuboresha maendeleo ya watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kupatiwa vitambulisho vya Taifa vitakavyowasaidia katika shughuli zao mbalimbali. Aidha amezitaja faida za kupatiwa vitambulisho vya Taifa kuwa ni kurahisisha upatikanaji wa huduma zote za msingi, kumtambulisha mtu mwenye ulemavu anapohitaji huduma, kumuwezesha kujidhamini kama anahitajika kufanya hivyo, kurahisisha zoezi la kuhesabu watu, pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa watu wenye ulemavu. Naye Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Wilaya ya Kinondoni, Bi.Subira Semsimbazi alipokuwa akitoa salaam za shukrani kwa Mkuu huyo wa Wilaya, ameainisha changamoto zinazowakabili kuwa ni ukosefu wa ofisi, ukosefu wa wakalimani, kutopatiwa huduma za bima afya, na pia kutopatiwa mikopo ya wanawake na vijana ili waweze kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali. Zoezi hili la utambuzi na usajili wa watu wenye ulemavu kwenye daftari la Taifa, kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya Taifa linafanyika kwa siku tatu katika shule ya msingi Ndugumbi iliyoko Manispaa ya Kinondoni. Imeandaliwa na Kitengo cha Uhusiano na Habari. Manispaa ya Kinondoni. WITO WATOLEWA KWA WANANCHI WAISHIO NA WATU WENYE ULEMAVU WILAYA YA KINONDONI Posted On: September 12th, 2018 KUHAKIKISHA WANASHIRIKIANA... + Read more »
ZOEZI LA UTOAJI WA ELIMU SAHIHI NA HUDUMA YA UZAZI WA MPANGO KWA JAMII LAENDESHWA MANISPAA YA KINONDONI Posted On: September 7th, 2018 NI KWA KUSHIRIKIANA NA SHIRIKA LISILO LA KISERIKALI LA JHPIEGO KUPITIA MRADI WA "TUPANGE PAMOJA" LENYE OFISI ZAKE MIKOCHENI. Zoezi hilo lililoendeshwa kwa siku tatu kwa kushirikiana na shirika la JHPIEGO limehusisha utoaji wa Elimu sahihi ya uzazi wa mpango, huduma ya uzazi wa Mpango kwa njia za muda mfupi ,na muda mrefu na za kudumu, sambamba na huduma hizo pia zimejumuisha upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi, maambukizi ya vvu, pamoja na shinikizo la damu, kwa Kata tano Kati ya Kata ishirini(20), za Manispaa hiyo. Akifafanua malengo ya zoezi hilo Mratibu wa huduma za Afya ya uzazi, na Mtoto wa Manispaa ya Kinondoni Bi.Edith Manase Mboga amesema lengo ni kuhakikisha elimu sahihi juu ya maswala ya uzazi wa mpango inawafikia wananchi bila kupotoshwa, ikienda sambamba na ongezeko la matumizi sahihi ya njia za uzazi wa mpango Ameongeza kuwa kwa kushirikiana na shirika la JHPIEGO chini ya mradi wa "TUPANGE PAMOJA" wamehakikisha Elimu sahihi, huduma ya uzazi wa Mpango,ushauri na upimaji wa magonjwa hayo inatolewa bure kwa wananchi. Katika zoezi hilo lililohusisha Kata ya Hananasif, Magomeni, Tandale, Kunduchi na Mwananyamala, mratibu huyo amewataka wananchi kuwa na utaratibu wa kutumia njia za uzazi wa mpango, kupima afya zao mara kwa mara ili kuweza kutambua muenendo wa mwili Kiafya na kuchukua hatua stahiki pindi inapohitajika. Imeandaliwa na Kitengo Cha Habari na Uhusiano Manispaa ya Kinondoni. ZOEZI LA UTOAJI WA ELIMU SAHIHI NA HUDUMA YA UZAZI WA MPANGO KWA JAMII LAENDESHWA MANISPAA YA KINONDONI Posted On: September 7th, 2018 ... + Read more »