KINONDONI YAPONGEZWA KUONGOZA MARA NNE MFULULIZO KIMKOA Posted On: February 24th, 2020 NI KATIKA KUFANYA VIZURI KWENYE MATOKEO YA KIDATO CHA NNE CHA PILI Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ,imepongezwa kwa kufanya vizuri katika matokeo ya kidato Cha nne na cha pili kwa miaka minne mfululizo kwa mkoa wa Dar es Salaam. Pongezi hizo zimetolewa na Afisa Elimu wa mkoa wa Dar es Salaam Bwana Hamis Lissu wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa walimu na shule zilizofanya vizuri kwa matokeo hayo kitaifa na kimkoa kwa mwaka 2019 ,2020. Lissu amesema kuwa Halmashauri hiyo imekuwa ikifanya vizuri na kwa ufanisi mkubwa kwa kila eneo ikiwemo Elimu, Afya na mazingira, Michezo na maeneo mengine na kusema kuwa mafanikio hayo yanatokana na kuwa na Mkurugenzi mwenye juhudi za kufanya kazi inayoendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano inayo ongozwa na Dk. John Pombe Magufuli. Lissi amefafanua kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unajumla ya Halmashauri tano lakini Halmashauri ya Kinondoni inayo ongozwa na Mkurugenzi wake Aron Kagurumjuli imekuwa ikifanya vizuri katika sekta ya elimu ambapo imeongoza kuwa na matokeo mazuri kwa miaka minne mfululizo katika mkoa huo. " Kinondoni imekuwa ikifanya vizuri sana kwenye mambo mengi, binafsi mnanikosha na utendaji wenu uliotukuka ,niwasihi nguvu hii mliyokuwa nayo muendelee nayo ili kuendelea kuwa na rekodi nzuri kwa kuwa mfano bora kwa Halmashauri nyingine zilizopo katika mkoa wetu" amesema Bwana Lissu. Lakini pongezi hizi pia zimuendee zaidi Mkurugenzi Kagurumjuli, Kinondoni mmepata Mkurugenzi bora, anafanya vizuri sana kwenye Halmashauri yake,na uchapakazi huu ndio anaoutaka Mhe. Rais wetu Dk. Magufuli, tukiwa na wachakazi kama hawa, hakika kwenye mkoa wetu tutakuwa na matokeo makubwa zaidi kwenye kila eneo” ameongeza Bwana Lissu. Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari, wa Halmashauri hiyo, Bwana Leornad Msigwa amesema katika matokeo ya kidato cha nne Kinondoni ilishika nafasi ya 39 kati ya Halmashauri 195 na hivyo kufanya kupanda nafasi tatu kitaifa ukilinganisha na mwaka 2018 ambapo ilishika nafasi ya 42 na kuendelea kuongoza kwa kishindo kwa miaka mine mfufulizo katika mkoa wa Dar es Salaam. Msigwa ameongeza kuwa tathmini ya matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2019 inaonyesha kuwa ufaulu umeongezeka kwa silimia 0.59 ukilinganisha na mwaka 2018 ambapo ufaulu umekuwa kwa asilimia 81.21 ambapo mwaka 2019 ufaulu ulikuwa kwa asilimia 81.80. Kwa upande wa matokeo ya kidato cha pili , Msigwa ameeleza kuwa tathmini ya upimaji wa matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka 2019 , ufaulu ulikuwa kwa silimia 94.04 na hivyo kufanya Halmashauri ya Kinondoni kushika nafasi ya 24 kitaifa kati ya Halmashauri 184 na hivyo kupanda nafasi 10 kitaifa ukilinganisha na mwaka 2018. Msigwa amefafanua kuwa, katika matokeo hayo mwaka 2019 watahiniwa walikuwa 9,340 ambapo waliofaulu mtihani huo kati ya daraja 1-1V walikuwa 8,783 sawa na asilimia 94.04. Amefafanua kuwa kati yao waliopata alama za ufaulu wa daraja la kwanza ni 1,682, daraja la piIi ni 1,216, daraja la tatu 1,556, daraja la nne 4,329 huku jumla ya watahiniwa 557 walipata alama ya sifuri. Katika hatua nyingine Msigwa amewaeleza walimu wa shule za Sekondari waliokuwa katika hafla hiyo kuendelea kujituma zaidi kwa kutumia mbinu mbalimbali za ufundishaji ili kuwezesha Halmashauri hiyo kuendelea kufanya vizuri zaidi kitaifa na kimkoa. Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Uhusiano Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. KINONDONI YAPONGEZWA KUONGOZA MARA NNE MFULULIZO KIMKOA Posted On: February 24th, 2020 NI KATIKA KUFANYA VIZURI KWENYE MATOKEO YA KIDAT... + Read more »