"TENGENEZENI MPANGO WA UWASILISHAJI MADA ZA AFYA ZINAZOISHI, KWENYE KILA MKUTANO WA WANANCHI UNAOFANYIKA Posted On: August 29th, 2018 Ni agizo lake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Daniel Chongolo, alipokuwa akitoa maelekezo, katika kikao kazi cha Kamati ya Afya ya Msingi ya Wilaya, kilichofanyika leo kwa lengo la kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za Afya, ikiwemo utekelezaji wa kampeni ya ugawaji dawa kinga na tiba kwa magonjwa ya kichocho na Minyoo ya tumbo kwa wanafunzi wa shule za awali na msingi. Amesema mada zinazoishi kuhusiana na masuala ya magonjwa ya jumla yanayoweza kuzuilika, ni kitu ambacho mwananchi anatakiwa kukumbushwa mara kwa mara kupitia watendaji ngazi ya Kata na Mitaa kwani asilimia kubwa yanatokana na uchafu na mazalia ya mbu. "Nitoe Rai idara ya Afya, tusisubiri dharura kwenye kushughulikia magonjwa ya mlipuko, katika vikao vyenu, ngazi za Kata,Mikutano ya wananchi, tengenezeni mpango wa uwasilishaji mada zinazoishi, mada inayoishi katika magonjwa ya jumla kama kipindupindu, kichocho, kwani haya msingi wake ni uchafu" Amebainisha Mh.Chongolo. Awali akimkaribisha Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dr. Festo Dugange amesema, Manispaa ya Kinondoni inavyo vituo 187, vya kutolea huduma za Afya vikihusisha hospitali, zahanati, kliniki, na martenity home ambavyo, kati yake 27 ni vya Serikali, na 160, ni vya binafsi, taasisi za Serikali, na Mashirika ya kidini tunavyoshirikiana navyo katika kuboresha utoaji huduma za Afya, ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zinazojitokeza, na kuweka mikakati ya maboresho katika sekta hiyo. Akitoa taarifa ya kampeni ya ugawaji wa dawa kinga na tiba kwa magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo kwa wanafunzi wa shule za awali na Msingi, mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Dr. Neema Mlole amesema, Kinondoni imelenga kufikia wanafunzi 121,086 , wenye umri kuanzia miaka 5 hadi 14, walioandikishwa katika shule za awali na Msingi, 157, zilizopo ndani ya Kata 20 za Manispaa ya Kinondoni. Ameongeza kuwa, katika kampeni hii, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya maendeleo ya jamii, jinsia ,wazee na watoto kupitia kitengo cha Mpango wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele imeshachukua hatua stahiki kuelekea kwenye utekelezaji ikiwemo kutoa elimu kwa wazazi na walezi, kutoa elimu kwa wagawa kinga tiba hizo watakaoshiriki zoezi, kusambaza dawa na vifaa maalumu, pamoj na mpango wa kuandaa chakula kwa wanafunzi kabla ya kuwapa kinga tiba hizo. Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya, kwenye kikao hicho kilichohusisha Kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya, wawakilishi wa mashirika ya dini, pamoja na wajumbe wa kamati, ameitaka idara ya Afya kuhakikisha inashughulikia maduka ya dawa muhimu, pamoja na hospitali bubu zinazoendeshwa bila vibali wala utaratibu, ili kujiepusha na madhara ya kiafya yanayoweza kutokea kwa watumiaji. Imeandaliwa na Kitengo cha Uhusiano na Habari. Manispaa ya Kinondoni. "TENGENEZENI MPANGO WA UWASILISHAJI MADA ZA AFYA ZINAZOISHI, KWENYE KILA MKUTANO WA WANANCHI UNAOFANYIKA Posted On: August 29th,... + Read more »
KUELEKEA KAMPENI YA UTOAJI KINGA TIBA ZA KICHOCHO NA MINYOO YA TUMBO KWA MKOA WA DAR ES SALAAM Posted On: August 28th, 2018 KINONDONI YATOA MAFUNZO KWA WAALIMU WA AFYA MASHULENI, NA WATOA HUDUMA, YA JINSI YA KUENDESHA ZOEZI HILO SIKU YA ALHAMISI Kinondoni kupitia idara ya Afya kitengo cha magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, kimeendesha mafunzo ya siku moja kwa waalimu wa masuala ya Afya mashuleni, pamoja na watoa huduma kutoka vituo vya afya na zahanati za Serikali, wa jinsi ya kugawa kinga tiba kwa magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo, kwa wanafunzi kuanzia umri wa miaka mitano(5) hadi kumi na nne(14), kampeni inayotarajiwa kufanyika siku ya Alhamis. Akizungumzia dhumuni la mafunzo hayo, Msimamizi wa Kampeni ya magonjwa hayo kwa Manispaa ya Kinondoni Dr.Neema Mlole amesema, mafunzo haya yanalenga kuwaandaa,waalimu katika kufanikisha zoezi hilo, likienda sambamba na kuwafundisha vigezo vinavyotakiwa kuzingatiwa wakati wa utoaji wa kinga tiba hizo kwa wanafunzi, kadhalika na kuwapatia vifaa vikihusisha kipimo cha urefu, na dawa hizo kwa ajili ya utekelezaji. Amesema kuelekea siku ya Alhamisi ya tarehe 30/08/2018, Kinondoni inatarajia kutoa aina mbili za kinga tiba ambazo ni Prazguantel kwa magonjwa ya kichocho na Albendazol kwa Minyoo ya tumbo kwa wanafunzi takribani 121,086 kutoka shule 157, za Manispaa. "Kinga tiba zitakazotolewa ni mbili, ambazo ni albendazol kwa ajili ya minyoo, na Prazguantel kwa ajili ya kichocho. Katika dawa hizi kabla ya kumpatia mtoto vipo vigezo vinavyotakiwa kuzingatiwa ambavyo ni kwanza Mtoto awe amekula chakula na kushiba, na pia apimwe urefu kwani Prazguantel kwa ajili ya kichocho idadi ya vidonge vyake huzingatia urefu." Amefafanua Dr.Neema. Ameongeza kuwa ni muhimu kwa watoto hawa kupatiwa kinga tiba hizi ili waweze kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza, na kwamba dawa hizi hazina madhara yeyote kwa mwanadamu. Mafunzo haya yaliyofanyika katika ukumbi wa Matakatifu Yosefu Manzese yamehusisha waalimu wa masuala Afya na watoa huduma vituo vya Serikali takriban 500, kwa lengo la kufanikisha kampeni hiyo ya utoaji wa kinga tiba siku ya Alhamisi tarehe 30/08/2018. Imeandaliwa na Kitengo cha Uhusiano na habari. Manispaa ya Kinondoni. KUELEKEA KAMPENI YA UTOAJI KINGA TIBA ZA KICHOCHO NA MINYOO YA TUMBO KWA MKOA WA DAR ES SALAAM Posted On: August 28th, 2018 KINONDONI Y... + Read more »
KAMATI YA FEDHA NA UONGOZI MANISPAA YA KINONDONI, YAFANYA ZIARA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO Posted On: August 28th, 2018 Ziara hiyo iliyoongozwa na Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mh George Mangalu Manyama ambae pia ni Diwani wa Kata ya kigogo imepata fursa ya kukagua utekelezaji wa miradi minne ya maendeleo ikiwa ni kwa lengo la kujiridhisha ubora unaoenda sambamba na ukamilishwaji wake ikihusisha hatua za ukamilishaji pamoja na thamani ya fedha iliyotumika. Katika ziara hiyo iliyohusisha wajumbe wa Kamati hiyo ya fedha ambao ni Wah. Madiwani, wakuu wa idara na vitengo pamoja na wataalam imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa madarasa manne shule ya msingi Mivumoni, ujenzi wa barabara ya Makanya iliyoko Tandale, ujenzi wa mfereji wa maji ya mvua barabara ya Ntuze iliyoko Kinondoni, pamoja na ujenzi wa Zahanati ya Mikoroshini iliyoko Kata ya Msasani. Mh Mangalu amesema hatua iliyofikiwa miradi hii ni nzuri na ya kuridhisha, inayoonesha mwelekeo wa dhamira ya dhati ya utekelezaji na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo itakayotoa huduma bora kwa Wananchi. "Miradi hii ni mizuri, na inaridhisha, tuhakikishe inamalizwa kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma bora katika jamii" Amesema Mh.Mangalu. Aidha amewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanaitunza na kuithamini miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao, ikiwa ni pamoja na kuwa walinzi wa uchafuzi wa mazingira na kuhakikisha wanaitunza mitaro ili iweze kutumika kwa makusudi kamili. Imeandaliwa na Kitengo cha Uhusiano na Habari. Manispaa ya Kinondoni. KAMATI YA FEDHA NA UONGOZI MANISPAA YA KINONDONI, YAFANYA ZIARA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO Posted On: August 28th, 2018 Ziara hiyo ili... + Read more »
MISINGI YA HAKI NA WAJIBU, NDIO NGUZO PEKEE YA MAFANIKIO KWENYE UTUMISHI WA UMMA" Posted On: August 24th, 2018 Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mh. Daniel Geofrey Chongolo alipokutana na watendaji wa Kata na Mitaa, pamoja na wakuu wa idara na vitengo, katika kikao kazi kilichofanyika ukumbi wa Oysterbay shule ya Msingi leo. Amesema kila, mtumishi wa Umma anao wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa wakati kwa kusimamia misingi ya sheria, kanuni na taratibu , ili kuepukana na migogoro inayoweza kuzuilika kwa mara moja. "Sisi tukitimiza wajibu wetu, kwenye maeneo yetu, hakuna mtu atakayepeleka malalamiko Wilayani, Mkurugenzi weka utaratibu wa kila mtu kuwa part and parcel ya eneo lake la kazi" Amesisitiza Mh.Chongolo. Kadhalika, amewataka watendaji wa Kata na Mitaa kuwa mstari wa mbele katika Kuzuia na kuepusha migogoro ya Ardhi, kuwa mstari wa mbele kukusanya mapato, kusimamia maswala ya usafi, na kujiepusha na viashiria vya rushwa. Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Ndg Aron Kagurumjuli, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mada za kikao kazi hicho, ameahidi kutekeleza maelekezo na maagizo yaliyotolewa na Mkuu huyo wa Wilaya, kwa kuwataka watendaji wa Kata na mitaa kuwa na takwimu sahihi za maeneo yao zikihusisha taarifa za wakazi, wafanyabiashara, masoko, maeneo ya uvuvi kwa waliopakana na bahari, wafugaji waliopo na aina ya mifugo wanayofuga, pamoja na takwimu sahihi za vibali vya ujenzi. Pia amewataka watendaji hao kuhakikisha wanazingatia misingi na mkondo wa mawasiliano ulio sawia, wanajiepusha na migogoro ya kiutendaji, na kuzungukia maeneo yao ya kazi na si kukaa ofisini. Aidha katika kikao kazi hicho, kilichoshirikisha wataalam kutoka sekta ya afya, biashara, mifugo, uchumi, Utumishi, kilimo, na elimu, kitaendesha mada sita ambazo ni wajibu na majukumu ya watendaji wa Kata, Usimamizi wa uendelezaji wa Miji, Usimamizi na uendelezaji wa daftari la mfanyabiashara, hatua sahihi za uanzishwaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na taratibu za manunuzi. Hii ni mara ya kwanza kwa Mkuu huyo wa Wilaya kukutana na Watendaji wa Kata na Mitaa wa Manispaa ya Kinondoni tangu kuteuliwa kwake kuitumikia Wilaya hiyo. Imeandaliwa na Kitengo cha Uhusiano na Habari. Manispaa ya Kinondoni. MISINGI YA HAKI NA WAJIBU, NDIO NGUZO PEKEE YA MAFANIKIO KWENYE UTUMISHI WA UMMA" Posted On: August 24th, 2018 Kauli hiyo imetolew... + Read more »