WATENDAJI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO NA MSHIKAMANO ILI KUKAMILISHA MIRADI ITAKAYO SOGEZA HUDUMA KWA WANANCHI
Posted On: October 1st, 2019
Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe Daniel Chongolo alipokuwa kwenye ziara ya kutembelea Miradi ya ujenzi wa Zahanati wilayani hapa.
Akiongea na wajumbe wa kamati ya kuratibu ujenzi wa Zahanati ya Makumbusho Mhe Chongolo amesema kuwa, kila hatua inatakiwa iwe na ushirikiano bainifu na wenye uwazi ambao hauwezi kuleta wasiwasi kwa yeyote.
"Hawa Wananchi tunaowahudumia msiwaone kama vile hawajui kitu, wanauelewa na uzoefu uliotukuka, wengine ni mafundi na wajua gharama za vifaa vya ujenzi", Ameongeza Mh Chongolo.
Mhe Chongolo amesema kuwa Zahanati za Magomeni na Makumbusho zitasaidia kupunguza msongamano uliopo Mwananyamala na hata ule ambao ungeweza kutokea katika hospitali ya wilaya inayojengwa Mabwepande baada ya kukamilika kwake.
Katika hatua nyingine Mh Chongolo ametoa siku 25 kwa mjenzi wa Zahanati ya Magomeni awe amekamilisha hatua ya awali pasipo kuchelewa maana Wananchi wanahitaji kusogezewa huduma ya afya karibu.
"Sisi tumepewa jukumu la kuhakikisha ilani ya chama cha mapinduzi inatekelezwa pasipo na dosari yoyote, kesho na keshokutwa hatutakuwa tayari kujibu maswali yenye majibu yake leo" Amesema Mh Chongolo.
Miradi iliyotembelewa na mkuu wa wilaya katika ziara hiyo ni pamoja na ujenzi was zahanati za Magomeni na Makumbusho na Mradi wa Hospitali ya wilaya inayojengwa kata ya Mabwepande.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment