TIMU MKAKATI YA KUJIANDAA KUKABILIANA NA MAAFA KINONDONI YATAKIWA KUJIKITA KATIKA KUZUIA MAAFA
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bi Sipora Liana alipokutana na timu mkakati ya kukabiliana na maafa yenye wataalamu 27 kwa lengo la kujadili mstakabali wa maafa katika kikao kilichofanyika ukumbi wa DMDP Kinondoni.
Amesema lengo ni kukumbushana Majukumu yanayowapasa kama wataalamu kufanyika ikiwemo kuweka mikakati ya kutoa elimu zaidi ya namna ya kuzuia ama kuepuka maafa hali itakayopelekea kupungua kwa madhara makubwa pindi yakitokea.
"Sitaki kusikia mafuriko Kinondoni, wananchi wanapokaa mabondeni waelimishwe na uzuri huwa wanajua chanzo kinachopelekea mafuriko kwenye maeneo yao, hivyo shirikianeni nao katika kuzuia mafuriko yasitokee badala ya kusubiri janga la mafuriko litokee ndio timu ianze kuhangaika" Ameongeza Bi Sipora.
Naye Mratibu wa maafa Manispaa ya Kinondoni Bi Pendo Mwaisaka alipokuwa akizungumza amebainisha maeneo ya awali yatakayopitiwa na Timu hiyo ya wataalam kutoa elimu kuwa ni maeneo ya huduma za Jamii kama Vituo vya kulelea watoto wadogo mchana na shule za Msingi na sekondari kufuatia kuripotiwa kwa changamoto za mara kwa mara za milipuko ya Moto.
Timu hiyo ya kukabiliana na maafa imehusisha wataalamu kutoka Idara na vitengo vya maendeleo ya jamii, Elimu Msingi na sekondari, Masoko,Takwimu Ugavi, Sheria,Ujenzi, Biashara, Tehama, Utumishi, Afya , Mazingira pamoja na Mipango Miji.
Wengine ni wataalam na wadau kutokaTanesco, jeshi la zimamoto na uokoaji, Jeshi la polisi , wakala wa mabasi yaendayo haraka (DART) Na TARURA
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment