DC CHONGOLO AWAONYA WAKUU WA SHULE ZA SEKONDARI KINONDONI
Posted On: January 17th, 2020
NI KUHUSIANA NA TARATIBU ZA KUWAPOKEA WANAFUNZI KIDATO CHA KWANZA.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo amewaagiza wakuu wa shule zote za Sekondari katika Wilaya hiyo kuacha mara moja tabia ya kuwazuia wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza kuanza masomo kutokana na kutokamilisha mahitaji yao ya shule.
Ametoa agizo hilo jana wakati wa sherehe za kuwapongeza walimu kwa ufaulu mzuri wa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2019 ambapo Kinondoni imepata ufaulu wa asilimia 97.17 na kuwa ya tatu kati ya Halmashauri 186 kitaifa, hafla iliyofanyika ukumbi wa officers Mess
Amesema kuwa zipo baadhi ya shule ambazo zinawazuia wanafunzi kujiunga na masomo kwa kile wanachokidai kutokamilisha mahitaji ya shule na kuzitaka shule za Kinondoni kutojihusisha na tabia hiyo bali kuwa sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano inayotekeleza sera madhubuti ya elimu bila malipo inayoenda sambamba na uchumi wa viwanda.
“Kuna baadhi ya maeneo nimesikia kuna wakuu wa shule wanawarudisha nyumbani watoto kwa sababu hawajakamilisha mahitaji yao, kama mtoto hana viatu, sijui nini waache wasome wakati wazazi wao wanawatafutia mahitaji hayo, naomba nisi sikie mwanafunzi amerudishwa nyumbani kwenye wilaya yangu” amesisitiza Mhe. Chongolo.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe. Benjamini sitta amesema kuwa mafanikio ya kufanya vizuri kwa wanafunzi wa darasa la saba mwaka 2019 kwenye Halmashauri hiyo ni uthibitisho tosha unao onesha namna walimu, wazazi na wanafunzi wanavyoshirikiana kikamilifu katika nyanja ya elimu na hivyo kutoa wito kwa wazazi kuendeleza ushirikiano huo katika usimamizi wa wanafunzi hususani kwenye masuala ya taaluma.
Kaimu Afisa elimu wa Halmashauri hiyo, Bi Chitegets Dominick pia alifafanua jumla ya wanafunzi waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa 12,619, wavulana 6,115 na wasichana 6,450, huku walioganya wakiwa 12,523, wavulana 6,058 na wasichana 6,465.
Katika hatua nyingine Mhe. Chongolo amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ndugu Aron Kagurumjuli kwa usimamizi mzuri wa elimu na kwamba anatambua jitihada zake za kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata elimu bila malipo na kwamba anatimiza kimamilifu majukumu na maagizo yanayotolewa na Rais Dk. John Magufuli
Imeandaliwa na
Kitengo cha na Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment