KINONDONI YAANZA RASMI MABORESHO YA UFUKWE COCOBEACH
Posted On: September 17th, 2019
Manispaa ya Kinondoni imeanza rasmi utekelezaji wa maboresho ya fukwe wa Cocobeach kwa kuikabidhi kampuni ya Tanzania Building works shughuli hizo za uendelezaji kwa mujibu wa makubaliano na michoro iliyopitishwa kisheria kwa ajili ya utekelezaji, ili iweze kutumiwa na watanzania kwa makusudi tarajiwa pindi itakapokamilika.
Akiongea mara baada ya kukabidhi fukwe hiyo kwa ajili ya maboresho Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Benjamin Sitta amesema, mradi wa Cocobeach ni mradi wa kimkakati hivyo Manispaa imefuata taratibu zote za kisheria hadi kufikia mchakato rasmi ambao umekabidhiwa kwa ajili ya utekelezaji.
"Kwa dhati ya moyo wangu niishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais wetu Mhe. Dr.John Pombe Magufuli kwa kuwajali watanzania na kuwaboreshea maeneo ya kupumzika, lakini pia kutupatia fedha za kuendeleza fukwe hii ya Cocobeach ambayo ni mradi wa kimkakati ili Halmashauri pia ziweze kujiendesha katika baadhi ya mambo, hii ni fursa pekee kwa Manispaa yetu ya Kinondoni kuhakikisha tunamuunga mkono Mhe. Rais kwa utekelezaji kwa kiwango kilichokusudiwa." Amefafanua Meya Sitta.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ndg Aron T Kagurumjuli amesema uendelezaji wa mradi huu wa kimkakati wa fukwe pamoja na miradi mingine katika Manispaa yake imefuata taratibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kumpatia mkandarasi mzawa jukumu hili, hali inayozingatia uzalendo na kuwataka watumiaji wa ufukwe huo kuwa sehemu ya uendelezaji kwa kuonesha ushirikiano pale inapopasa hasa uvumilivu katika kipindi hiki cha maboresho na kurejea pale itakapokamilika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Tanzania Building Works ndg Iqbal Noray ameishukuru Manispaa na Serikali kwa ujumla kwa kuwaamini na kuahidi kuikamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi kilichopangwa kwa weledi na ubora uliokusudiwa.
Imeandaliwa na
Kitengo cha
Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment