JAMII YATAKIWA KUJENGA MAZOEA YA KUCHANJA MBWA NA PAKA ILI KUWAKINGA DHIDI YA UGONJWA HATARI WA KICHAA CHA MBWA
Posted On: September 28th, 2019
Wito huo umetolewa na Tabibu wa mifugo mkoa wa Dar es salaam Dr Senorina Mwingira katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kichaa cha Mbwa Duniani yanayofanyika kila Tar 28 Septemba ambayo kwa wilaya ya Kinondoni yamefanyika viwanja vya Mbezi Ndumbwi.
Dr Senorina amesema Kichaa cha mbwa ni hatari sana kwa binaadamu na wanyama kwani hakina tiba zaidi ya kinga hivyo niwapongeza sana Kinondoni kwa hamasa yenu kuhamasisha wananchi kuchanja Mifugo yao kwani si tu mnailinda jamii bali mnalinda haki za wanyama hawa pia.
Naye Afisa Mifugo toka wilaya ya Kinondoni Bi Bertilla Lyimo kwa niaba ya Mkuu wa idara ya Mifugo wa Manispaa hiyo amesema chanjo hiyo itakuwa endelevu na zoezi hilo litafanyika kata kwa kata hivyo amewasihi wanajamii ya Kinondoni kufanya mwendelezo wa chanjo hii kwa manufaa yao na wanyama wao.
Aidha amebainisha kuwa, waathirika wakubwa wa athari za kichaa cha mbwa ni watoto chini ya miaka 15, hivyo jamii itakapochukua hatua stahiki itakuwa imewalinda wahanga hao ambao ni watoto.
Katika hatua nyingine kabla ya maadhimisho hayo, Manispaa ya Kinondoni ilionesha onesho la sinema kwa wanafunzi zaidi ya 800 toka shule ya msingi Mbezi Ndumbwi linaoelezea madhara ya ugonjwa wa Kichaa cha mbwa kwa binaadamu, ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa wanafunzi hatua za kuchukua endapo itatokea akang'atwa na mbwa au paka ili asiweze kupata ugonjwa hatari wa kichaa Cha mbwa.
Manispaa ya Kinondoni imelenga kuchanja mbwa takribani 1342 na paka 246 katika kata zote 20 na hii ni dhamira ya kuendana na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo "UGONJWA WA KICHAA CHA MBWA: CHANJA MIFUGO YAKO ILI KUTOKOMEZA UGONJWA HUU(RABIES VAAACCINATE TO ELIMINATE)
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni
0 comments:
Post a Comment