KINONDONI YAENDESHA SEMINA ELEKEZI KWA WENYEVITI NA MAKATIBU WA KAMATI ZA USIMAMIZI WA MAAFA ZA KATA.
Posted On: May 25th, 2019
NI KUHUSIANA NA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA MAAFA YA MWAKA 2015 NA JINSI YA KUKABILIANA NA MAJANGA KATIKA SEKTA HIYO.
Akifungua semina hiyo leo katika ukumbi wa DMDP jijini Dar es salaam, Mkuu wa idara ya Mendeleo ya Jamii Bi.Halima Kahema amesema, lengo ni kuzijengea uwezo kamati za kata kwani ndio msingi mzima katika kutekeleza sera na usimamizi wa sheria hii ya maafa ya mwaka 2015, ngazi ya Kata na Mitaa.
Ameongeza kuwa ili uweze kutekeleza Jambo ni lazima ulijue, na katika hili ni dhahiri kabisa mana kunapokosekana usimamizi mzuri unaoenda sambamba na utekelezaji wowote wa sheria hakika zoezi linakuwa gumu, na hata uchukuaji wa hatua stahiki katika sekta hiyo pia unakuwa mgumu.
Bi. Halima amesema "wenyeviti na makatibu wa Kamati mnatakiwa kwanza kuijua sheria vizuri ili muweze kuwa na maamuzi na mamlaka kamili katika kutafuta njia nzuri zaidi za kukabiliana na maafa pale yatakapojitokeza".
Aidha mratibu wa Maafa Manispaa ya Kinondon Bi. Pendo Mwaisaka wakati akiongea,ametoa msisitizo wa utoaji wa taarifa kwa wakati, na taarifa hizo ziambatane na takwimu sahihi la tukio husika na kusisitiza kuwa suala la Maafa ni suala mtambuka linalohitaji nguvu ya pamoja na Serikali, sekta binafsi na wadau wengine.
Mada zilizowasilishwa katika semina hiyo ni Mpango wa kukabiliana na dharura mkoa wa Dar es salaam, Jinsi ya kuandaa mipango ya kujiandaa na kupunguza athari za majanga, Uokozi na namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali, maafa, majanga na uokozi na nini kifanyike kukabiliana na majanga.
Nyingine ni miradi inayotekelezwa na Manispaa ya Kinondoni DMDP iliyolenga kupunguza athari za mafuriko, sheria ya usimamizi ya maafa ya mwaka 2015 pamoja na utoaji wa taarifa za majanga.
Semina hii imepata uwakilishi kutoka DarMAERT, oxford policy, Chama cha msalaba mwekundu, na Jeshi la zimamoto, na kuhudhuriwa na maafisa watendaji wa kata, maafisa maendeleo ya jamii Kata pamoja na wadau wengine.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment