TAMISEMI YAENDESHA MAFUNZO YA SIKU MOJA KWA KAMATI YA LISHE KINONDONI
Posted On: November 16th, 2018
NI KUHUSIANA NA UANDAAJI WA MIPANGO YA HUDUMA ZA LISHE KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020.
Ofisi ya Raisi -TAMISEMI kupitia kitengo cha lishe imeendesha mafunzo kwa Kamati ya lishe ya Manispaa ya Kinondoni, yahusuyo mipango ya utekelezaji wa huduma za lishe kwa watoto umri chini ya miaka mitano, ikiwa ni pamoja na kuongeza uelewa katika swala zima la utekelezaji wake, hasa uwekaji wa vipaumbele katika bajeti ya 2019/2020.
Akifungua mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Manispaa, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bi Stella Msofe amesema mafunzo haya ni muhimu, na yakawe chachu ya utekelezaji wa jambo hili, hasa ikizingatiwa azma ya Serikali ni kuhakikisha inaepukana na madhara yanayoweza kutokea kwa watoto wetu pindi wanakosa lishe bora
Naye mkufunzi kutoka ofisi ya Rais -TAMISEMI Bi.Mary Kibona, alipokuwa akiwasilisha mada ihusianayo na mpango mkakati wa utekelezaji,amefafanua maana halisi ya lishe kuwa ni mchakato wa tangu chakula kinapoliwa mdomoni, kinasagwa na kuingia mwilini na kuanisha madhara ayapatayo mtoto anapokosa lishe bora kuwa ni kupata upungufu wa madini na Vitamini mwilini.
Akiainisha mafanikio ya Kamati ya lishe kwa Manispaa ya kinondoni tangu kuundwa kwake, Afisa lishe wa Manispaa hiyo Bi Emiliana Sumaye amesema , kamati hiyo imefanikiwa kupeleka shughuli za lishe kwa idara mtambuka, imefanikiwa kukaa vikao vitatu vya kujadiliana mwelekeo mzima wa lishe na kuainisha njia sahihi za kuhakikisha lengo linafikiwa, imefanikiwa pia kuhakikisha vituo 65 vya kutolea huduma za afya vilivyoko Manispaa vinatoa elimu ya lishe, na kufikia wazazi takribani 19,399 kwa elimu hiyo ya lishe kwa watoto na wajawazito.
Pia ameainisha changamoto zinazowakabili kuwa ni Jamii kushindwa kutumia huduma ya uzazi kikamilifu, watoa huduma kutowajibika ipasavyo, kuwepo na upungufu wa watoa huduma ngazi ya jamii, na watoa huduma kutopata elimu ya utoaji wa vidonge vya folic Acidi.
Mafunzo haya yaliyohudhuriwa pia na wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkoa wa Dar es salaam Bi Janeth Mzava, Mwakilishi kutoka, UNICEF Bi.Joyce Ndeba, Mwenyekiti wa huduma za Uchumi Afya na Elimu Mh.Thadei Masawe, kamati ya lishe ya Manispaa, pamoja na wakuu wa idara na vitengo, yamejadili mada zihusuzo uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa shughuli za lishe.
Nyingine ni Mpango na bajeti ya lishe kwa kutumia planrep, shughuli za lishe/afua za lishe zinazoweza kupangwa ngazi ya vituo vya afya na upatikanaji wa rasilimali watu na fedha.
Imeandaliwa na,
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment