MKURUGENZI KINONDONI AWATAKA BVR KITS OPERATORS, KUZINGATIA KANUNI NA TARATIBU ZA UBORESHAJI DAFTARI AWAMU YA PILI
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeanza zoezi la uboreshaji awamu ya pili wa daftari la kudumu la mpiga kura ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambaye ndio Afisa mwandikishaji bwana Aron Kagurumjuli amesema wamejipanga vilivyo katika uboreshaji huo.
Kagurumjuli ametoa kauli hiyo wakati wamafunzo ya kuwajengea uwezo mbalimbali kuhusu namna ya kuwahudumia wananchi wanaokuja kuboresha taarifa zao sambamba na namna ya kutumia mashine wakati wa kuchukua picha kwa ajili ya kutoa vitambulisho.
Kagurumjuli amesema kuwa Halmashauri yake imejipanga vizuri katika mchakato huo na kwamba inategema matokeo mazuri ya mwitikio wa wananchi kama ilivyokuwa kwa awamu ya kwanza kutokana na kuwepo kwa ushirikiano madhubuti baina ya AROKATA pamoja na watendaji wengine wa Hamashauri hiyo.
Ameongeza kuwa mchakato huo ni mahususi kwa ajili ya kuwapatia wananchi vitambulisho vyao na kuwataka wale ambao walipitwa na mchakato huo kwa awamu ya kwanza kujitokeza sasa ili waweze kupata vitambulisho vyao.
“ Nawapongeza wote mliopata nafasi hii, kiapo mlichokula hapa ni cha uaminifu na uadilifu, mnakwenda kuwahudumia wananchi, niwasihi hatuhitaji muende kinyume na maelekezo ambayo mnapewa na watalaamu wetu kwenye mafunzo haya, wahudumieni wananchi vizuri” amesema Kagurumjuli.
Aidha Kagurumjuli amewataka watumishi hao kuzingatia maelekezo wanayopewa na watalaamu kuhusu namna ya kumuhudumia mwananchi hasa katika kipindi hiki cha ugonjwa wa mlipuko wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya COVID 19 (Corona) ikiwemo kunawa mikono na maji tiririka pamoja na kupaka vitakasa mikono (Sanitizer).
Amesema kuwa katika kila kituo kutakuwa na watu ambao watakuwa ni mahususi kwa ajili ya kuwanawisha mikopo pamoja na kuwapaka vitakasa mikono ili kuwakinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Kagurumjuli amefafanua kuwa zoezi hilo la uandikishaji litaanza rasmi Mei mbili na kumalizika Mei Nne mwaka huu na kwamba wote ambao hawakupata nafasi ya kujiandikisha awamu ya kwanza wanaruhusiwa kwenda kwenye vituo vyao kwa ajili ya kujiandikisha.
Imeandaliwa na
kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni
0 comments:
Post a Comment