DC CHONGOLO AKABIDHI MADARASA, OFISI ZA WALIMU KATIKA SHULE YA SEKONDARI TWIGA NA KIGOGO ,AMPONGEZA MKURUGENZI
Posted On: November 26th, 2019
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo amekabidhi madarasa sita na ofisi tatu za walimu katika Shule ya Sekondari Kigogo iliyopo Kata ya Kigogo na Shule ya Sekondari Twiga iliyopo Kata ya Wazo ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kujenga vyumba 100 vya madarasa ili kuondoa tatizo la wanafunzi wanaomaliza darasa la saba kukosa nafasi ya kwenda shule kwa changamoto ya upungufu wa madarasa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Chongolo amesema ujenzi huo unaendelea kwa juhudi zake binafsi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wapenda maendeleo katika wilaya yake, hivyo anawashukuru wadau hao walioshirikiana naye kwani kukamilika kwa madarasa hayo kutasaidia wanafunzi wote wanaomaliza darasa la saba kuendelea na masomo ya Sekondari badala ya kukaa nyumba.
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli iliamua kutoa elimu bure kwa kila mmoja ili kuhakikisha kwamba hakuna mtoto anayekaa nyumbani bila kusoma na kwamba atahakikisha madarasa hayo yanakamilishwa ili kutimiza adhma hiyo.
Amefafanua kuwa kutokana na mpango wa elimu bure uliotolewa na Rais Dk. Magufuli kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wanaoandikishwa shule hivyo serikali itahakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kusoma wakiwa kwenye vyumba vya madarasa.
“ Awali tulikuwa na changamoto ya walimu lakini Mhe. Rais amehakikisha kuwa changamoto hiyo imekwisha ,hivi sasa tunachangamoto ya vyumba vya madarasa , hili nalo litakwisha, niwahakikishie serikali ya awamu ya tano ipo pamoja na wananchi wake” amesema Mhe. Chongolo.
Nakuongeza kuwa” leo hii nimekuja mwenyewe kuzindua madarasa haya ili kuona ufanisi uliopo, niseme tu kwamba nimeridhishwa na nimefurahi kuona madarasa haya yamekamilika, sasa imebaki viti na meza ili wanafunzi waweze kusoma na nimeambiwa tayari vimeshaagizwa.
Aidha amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Ndugu Aron Kagurumjuli kwa kuwa begakwabega na yeye katika kusimamia na kuhakikisha lengo la ujenzi wa vyumba 100 vya madarasa kwenye Halmashauri yake linatimia.
Katika hatua nyingine Mhe. Chongolo amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao kwani viongozi wamekuwa wakifanya jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba wanapata madarasa ya kusomea.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment