SERIKALI YAPONGEZA MAONESHO YA NANE NANE KANDA YA MASHARIKI
Posted On: August 8th, 2019
NI KUTOKANA NA JUHUDI WANAZOZIFANYA KATIKA KUINUA NA KUKUZA UCHUMI WA NCHI KUPITIA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan, alipokuwa mgeni rasimi katika kilele cha maadhimisho ya nane nane kanda ya Mashariki yaliyofanyika katika viwanja vya Mwl J K Nyerere Mkoani Morogoro.
Amesema ili Uchumi wa nchi ukue, tunategemea viwanda, na malighafi ambazo nyingi tunazipata mashambani, hivyo kwa kanda ya Mashariki inayohusisha mikoa ya Tanga, Pwani Dar es salaam na Morogoro kwa kauli mbiu isemayo "Kilimo, mifugo na uvuvi kwa ukuaji wa Uchumi wa nchi ", imetekelezeka.
"Tunapozungumzia suala la kukuza uchumi wa Nchi kama kauli mbiu yetu inavyoelekeza kwa mwaka huu tunahitaji kuboresha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, na hili nimeliona nilipotembelea mabanda mbalimbali hapa, nawapongeza kwa jitihada mnazofanya" amesema Mhe Makamu wa Rais.
Pamoja na kuwapongeza viongozi wanaounda ukanda huo, Makamu wa Rais amesisitiza pia juhudi hizo zisiishie kwenye mabanda ya nanenane pekee bali zifikie wananchi wote ambao wanatakiwa kuona mifano halisi kwa viongozi wao wanaowapa mafunzo.
Aidha katika maonesho hayo ya 26,Manispaa ya Kinondoni imeshika nafasi ya pili huku nafasi ya kwanza ikichukuliwa na Manispaa ya Ilala.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment