Top ad

Top ad

ELIMU YA AFYA, UZAZI NA UPIMAJI NA USHAURI NASAHA KWA WANANCHI YATOLEWA KINONDONI.

Posted On: June 7th, 2019
Kinondoni kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la JHPIEGO lenye kauli mbiu ya "TUPANGE PAMOJA"yaendesha zoezi la utoaji elimu ya Afya ya Uzazi, upimaji na ushauri nasaha kwa wananchi ili kulinda na kuboresha afya zao.
Akifafanua kuhusu zoezi hilo, lililofanyika katika mtaa wa Hananasif  Kinondoni, Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dr Festo Ndugange amesema kuwa kipaumbele cha serikali ya awamu ya tano ni kujenga na kukuza uchumi wa nchi kupitia Viwanda, katika kuhakikisha hilo linatimia wanahitajika watu wenye afya njema kimwili na kiakili ili waweze kutoa mchango utakiwao kwa wakati sahihi.
"Wakati viongozi wetu wanapigania masuala ya kukuza uchumi wanahitaji mwitikio chanya kutoka kwenye jamii na hilo linawezekana endapo jamii hiyo itakuwa na watu wenye afya njema na nguvu imara,  nasi tumeona namna nzuri ya kutoa mchango wetu ni kuwapa elimu, kinga na tiba imara wakati wote" ameongeza Dr Festo.
Akiongea katika zoezi hilo, mratibu wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto Manispaa ya Kinondoni Bi. Edith Manase Mboga amesema, huduma na elimu inayotolewa inalenga kupunguza au kumaliza kabisa matatizo yanayoikumba jamii hasa ikizingatiwa chanzo  chake ni ukosefu wa uelewa na kutokuwa na uthubutu wa familia kukaa na kuweka mikakati ya pamoja juu ya masuala ya afya.
Huduma walizopatiwa wananchi hao ni elimu juu ya afya ya uzazi, upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti, shinikizo la damu, ushauri nasaha na upimaji wa hiari wa VVU.
Wananchi waliojitokeza  katika zoezi hilo wameishukuru Manispaa ya Kinondoni kwa  fursa hiyo adimu itakayowawezesha kupata elimu juu ya mwasuala ya Afya ya uzazi pamoja na athari azipatazo mtu asiyefuata masuala hayo ya Afya.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.

0 comments:

Post a Comment

 
Top