RAI YATOLEWA KWA MASHIRIKA YA UMMA, NA BINAFSI KUSHIRIKI KAMPENI YA UCHANGIAJI UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA KINONDONI
Posted On: February 7th, 2019
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe Daniel Chongolo alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya upokeaji mifuko 200 ya simenti kutoka Shirika la Nyumba la Taifa.
Akipokea Mifuko hiyo ya simenti, Mh Chongolo amesema huo ni mfano wa kuigwa kwani kwa kufanya hivyo si tu kuunga mkono Halmashauri ya Kimondoni katika kampeni ya ujenzi wa vyumba 100, vya madarasa, bali pia ni kumuunga mkono Rais wa awamu ya tano, katika falsafa aliyonayo ya kuboresha mazingira ya elimu Nchini Tanzania.
Amesema "Wilaya yetu ya Kinondoni, imejiwekea lengo ya kwamba ifikapo mwezi wa tatu, tuwe tumekamilisha kujenga vyumba 40 kwa shule za sekondari, na vyumba 60 kwa shule za msingi, hali ambayo bila mashirika na taasisi binafsi kutuunga mkono si rahisi, kadhalika ni faraja kwetu sote kuona hali hii ya ushirikiano katika kuboresha miundombinu hii ya elimu inaendelea, kwani azma yetu ni kuona vijana wetu wanapatiwa mazingira rafiki ya kusomea na waalimu kufundisha" Mh Chongolo.
Naye kaimu mkuu wa kitengo cha huduma za jamii na mawasiliano kwa umma kutoka shirika la nyumba la Taifa Bw Yahya Charahani amesema elimu ndio ufunguo wa Maisha na ukitaka kumkomboa mtoto wa mwananchi aishiye chini ya dola moja yaani masikini mpatie elimu, na ndio maana tumefarijika sana kuungana na Halmashauri yetu hii katika kuhakikisha miundombinu ya elimu inaboreshwa na watoto wanasoma bila bugudha yeyote.
Kwa upande wake Afisa elimu sekondari Bw Leonard Msigwa alipotakiwa kuzungumza, amelishukuru shirika la Nyumba la Taifa kwa kujitoa kuchangia Ujenzi wa vyumba vya madarasa kwani kwa kukamilika kwake kutatatua changamoto iliyopo kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment