WAKULIMA KINONDONI WAMETAKIWA KUELEWA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI KATIKA SEKTA YA KILIMO ILI WAWEZE KUKABILIANA NAZO
Posted On: January 18th, 2019
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bi.Stella Msofe, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu yaliyoendeshwa katika kituo cha kilimo malolo kwa lengo la kutoa elimu mahususi juu ya mabadiliko ya tabia nchi katika sekta ya kilimo na jinsi ya kukabiliana nayo.
Amesema ni lazima wakulima hawa wapatiwe elimu ya kutosha itakayowawezesha kuepukana na athari hizo, kwani kilimo ndio uti wa Mgongo wa Taifa letu, hasa ikizingatiwa tunahitaji malighafi za kutosha kuendeshea viwanda vyetu, ambayo kwa sasa ndio sera ya Serikali ya awamu ya tano, Serikali ya viwanda.
Amesema "Bahati nzuri Kinondoni tunayohazina ya wataalam wa sekta hii, tunacho kituo bora kabisa kwa ajili ya elimu hiyo, kwanini tushindwe kutoa elimu kwa walengwa?, kwanini wakulima wetu wasipate elimu, wataalam hawa wapo, na wanalipwa kwa kazi hiyo, hivyo watumieni, kwani jukumu lao ni kurudisha ujuzi, elimu na maarifa kwa jamii husika." Bi.Msofe.
Awali akiainisha lengo zima la mafunzo hayo kwa Katibu Tawala huyo, Mkuu wa Idara ya kilimo na mifugo Manispaa ya Kinondoni, ambaye pia ni msimamizi wa kituo cha kilimo Malolo, Bw Salehe Hija amesema, mafunzo haya yaliyohusisha wakulima 40, kutoka Kata tano za Manispaa hiyo, yamelenga si tu kutoa uelewa, bali pia kuainisha njia sahihi za kupambana na changamoto zake, ili wakulima waweze kufanya kilimo chenye tija.
Amezitaja Kata zilizoshiriki mafunzo hayo kuwa ni kata ya Mbweni, Bunju, Mabwepande, Wazo na Kunduchi, na kuwataka wakulima hao kuwa mabalozi kwa wakulima wengine kwa elimu waliyoipata, ili elimu ienee na kuweza kuleta tija.
Akishukuru uongozi wa Manispaa ya kinondoni kwa kuendesha mafunzo hayo, kwa niaba ya wakufunzi wengine, Mwenyekiti wa wakulima waliopatiwa mafunzo hayo Bw John Malekela amesema elimu hii ni hazina tosha kwa sekta nzima kwa Wilaya yetu, kwani tunaahidi kuitendea kazi ili waweze kuepukana na changamoto hizo za mabadiliko ya tabia nchi na waweze pia kujiongezea thamani ya mazao yao.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment