Top ad

Top ad

KINONDONI YAAPISHA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA NA WAJUMBE WAKE

Posted On: December 2nd, 2019
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo amewataka Wenyeviti wa Serikali za mitaa kuwa wadilifu katika kuwatumikia wananchi walio wachagua na kwamba waepuke kuwa miungu watu.
Mhe. Chongolo ametoa kauli hiyo leo wakati wa hafla ya kuapishwa kwa viongozi wa serikali za mitaa wa Halmashauri hiyo na kueleza kuwa kuapishwa kwao leo hakuwafanyi wakawe miungu watu kwa wananchi badala yake wakawatumikie kwa uadilifu.
Ameongeza kuwa suala la maslahi binafsi haliruhusiwi katika utendaji wao na kwamba hategemei kuona wenyeviti hao wanakwenda kinyume na maelekezo yanayotolewa.
“ Mmekula kiapo cha kwenda kutenda haki majukumu ya kuwatumikia wananchi, hamjala kiapo cha kwenda kuwa miungu watu, kuwa wabaguzi, hamjala kiapo ili mkawe watu wa kupendelea baadhi ya watu, na kuonea wengine"
Aidha Mhe. Chongolo amewaeleza kuwa kuna changamoto ya uonevu wa nyumba na mali za wanyonge hivyo kuwataka viongozi hao wa mitaa wakasimamie changamoto hizo.
 “ Kuna wananchi wanatapeliwa nyumba zao  na wajanja wajanja , ili wajimilikishe wao, kuanzia sasa nitasikitika sana hasa nikitambua nyinyi ambao leo hii ninawashuhudia mkila kiapo hapa mnakwenda kufanya mambo haya , nawaonya awamu hii sitawaacha, hatuwezi kukaa na watu wa hovyo, narudia hatuwezi kukaa na watu wa hovyo” amesisitiza Mhe. Chongolo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa Ndugu. Aron Kagurumjuli amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa kutumia vizuri madaraka waliyopewa na wananchi ili kuepusha mitafaruku ambayo ilikuwa ikijitokeza kwa baadhi ya wenyeweviti waliomaliza muda wao.
Amefafanua kuwa kazi ya wenyeviti wa serikali za mitaa hazina mishahara na kwamba inahitaji uzalendo mkubwa hivyo kuwataka watumie nafasi zao vizuri ili waweze kuendesha shuguli zao kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi waliowachagua.
Aidha amewaonya wenyeviti hao kuacha mara moja tabia ya kuwatoza fedha wananchi pindi wanapotaka huduma  hivyo kuwaeleza kuwa huduma hizo zinapaswa kutolewa bure na kwamba atakayekwenda kinyume na maelekezo hayo hatamvumilia kwa namna yoyote ile.

Imetolewa na 
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
 Manispaa ya Kinondoni.

0 comments:

Post a Comment

 
Top