Top ad

Top ad

KINONDONI YAZINDUA KAMATI YA MAAFA YA WILAYA.

Posted On: November 22nd, 2018
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Daniel Chongolo leo,  amezindua kamati ya maafa ya Wilaya yenye wajumbe 29 ambapo wajumbe 18 ni kutoka timu ya Manispaa na wajumbe  11 ni wadau kutoka nje ya Halmashauri, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.
 Akizindua kamati hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya katika hotuba yake amesema,  maafa ni tukio kubwa linalotokea na kuathiri utaratibu wa maisha ya jamii na kusababisha madhara makubwa kwa watu, mali, uchumi na mazingira  ambapo huzidi uwezo wa jamii kukabiliana nalo.
 Ameongeza kuwa kwa Serikali kutambua uwepo wa maafa na majanga Nchini na umuhimu wa kukabiliana nayo,  imetunga sheria ya usimamizi wa maafa namba 7 ya mwaka 2015, inayotaka uundwaji wa kamati ufanyike, kwa lengo la kuchukua hatua za kujiepusha nayo na kukabiliana pindi yanapojitokeza.
 Amesema "Kamati ninayoizindua leo ni utekelezaji wa matakwa ya Sheria, hivyo hatupo hapa kwa bahati mbaya na kamati hii inatambulika kwa mujibu wa sheria tajwa, kifungu cha 15 na 16 hivyo nendeni mkafanye kazi" Amesisitiza Chongolo.

 Awali akisoma taarifa ya uundaji wa kamati ya usimamizi wa Maafa wa Wilaya kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa,  Mratibu wa Maafa wa Manispaa hiyo Bi.Pendo Fred amewataja wajumbe wanaounda kamati kuwa ni wakuu wa idara na vitengo 16 vya Manispaa, Jeshi la zimamoto na uokozi Mkoa wa Kinondoni, TARURA, TANESCO, DART,  DAWASCO na vyombo vya habari.
 Aidha ameainisha mipango na mikakati ya kamati kwa mwaka 2018/2019 kuwa ni kufanya mkutano na wadau, kutoa mafunzo kwa kamati za maafa ndani ya Mtaa na Kata, kuanzisha program ya kutoa mafunzo katika jamii na Halmashauri kutekeleza miradi ya DMDP kwa kujenga barabara zenye mifereji.
 Naye mratibu wa timu ya wataalam ya uokoaji ya Mkoa wa Dar es Salaam (DARMAERT),  Ndg Christopher Mzava, alipokuwa akitoa taarifa yake ameyaainisha majukumu ya kamati iliyozinduliwa kuwa ni kuhuisha masuala ya dharura na maafa katika mipango ya maendeleo, kufuatilia tishio la majanga na maafa na kufanya uchunguzi wa kutokea kwa maafa na uchoraji wa ramani.
 Nyingine ni kuainisha mahitaji ya mafunzo kwa umma na kutoa elimu, kutafuta rasilimali na kusimamia operesheni za maafa na kuunda timu ya ukabilianaji wa maafa na muundo wa kulinda jamii.
 Uzinduzi wa kamati hiyo pia umehudhuriwa na wawakilishi kutoka Bank ya Dunia, msalaba mwekundu, wawakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa na waheshimiwa madiwani.
 Imeandaliwa na 
 Kitengo cha Habari na Uhusiano. 
 Manispaa ya Kinondoni.

0 comments:

Post a Comment

 
Top