Top ad

Top ad

KINONDONI YAANDAA MAONESHO YA BIDHAA ZA NGOZI YATAKAYOFANYIKA VIWANJA VYA TANGANYIKA PACKERS

Posted On: December 10th, 2019
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo amesema kuwa katika kuhakikisha tunakuza uchumi wa Viwanda, Wilaya hiyo imeandaa maonesho ya wajasiriamali wa bidhaa za ngozi yatakayofanyika Disemba 12 hadi 15 katika viwanja vya Tanganyika Packers.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mhe. Chongolo amesema kuwa maonesho hayo ambayo yata ambatana na uuzaji wa bidhaa hizo yatafanyika ikiwa ni katika mkakati wa kutangaza na kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa zinazo zalishwa hapa nchini.
Amesema kuwa lengo la maonesho hayo ni kutangaza uwezo wa wadau wa ngozi, kuelimisha jamii kujenga utamaduni wa kutumia bidhaa hizo zenye ubora zinazozalishwa hapa nchini sambamba na kuongeza soko la ajira kwa vijana.
Amefafanua kuwa maonesho hayo yatahusisha wajasiriamali kutoka Wilaya ya Kinondoni pamoja na Halmashauri nyingine za mkoa wa Dar es salaam.
Mhe. Chongolo amefafanua kuwa kupitia sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Manispaa ya Kinondoni ina wakazi zaidi ya milioni 1.3, ambapo idadi hiyo inategemea kupata bidhaa za ngozi, ikiwemo Viatu, Mikanda, Mabegi na pochi zinazo tokana na bidhaa za ngozi.
Mhe. Chongolo ameeleza kuwa hali hiyo imekuwa tofauti kutokana na watu hao kutumia bidhaa zinazozalishwa kutoka nje ya nchi na hivyo kuwasihi wananchi kupenda kutumia bidhaa zinazo zalishwa hapa nchini.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi kubwa barani Afrika zinazo zalisha ngozi kwa kiasi kikubwa ,na ya Tatu miongoni mwa nchi zenye mifugo mingi barani Africa, pia Tanzania ni nchi ambayo inatumia bidhaa hizo kwa wingi, mfano takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya viatu zaidi ya milioni 53 zinaingia na kutumika kila mwaka” ameeleza Mhe. Chongolo.
Rais wetu mpendwa, Dk. John Magufuli kila siku amekuwa akisisitiza kujenga viwanda ili kufikia uchumi wa kati, na sisi wasaidizi wake tunaliangalia hilo kwa kulifanyia kazi, ndio mana tumeona tuwaweke pamoja wajasiriamali wa bidhaa za ngozi, na hatutaishia hapa tunampango mwakani tuyafikishe mbali zaidi” amesema Mhe. Chongolo.
Mhe. Chongolo amefafanua kuwa pamoja na kwamba Tanzania inazalisha ngozi nyingi lakini ipo changamoto kubwa inayotokana na malighafi hizo kusafirishwa nje ya nchi jambo ambalo amesema limesababisha kuwepo kwa uhaba wa ngozi kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa hizo.
Hata hivyo Mhe. Chongolo amesema kuwa maonesho hayo yenye kaulimbiu “Kinondoni yetu, Viwanda vyetu, Tanzania yetu” itakuwa ni fursa kwa vijana wengi kujiajiri , kuongeza pamoja na kukuza viwanda vya ndani vya ngozi na hivyo kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa hizo.
Imetolewa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.

0 comments:

Post a Comment

 
Top