Top ad

Top ad

DC KINONDONI ATOA SIKU SABA KWA WAKANDARASI WA TAKA KUBORESHA HUDUMA HIYO

Posted On: November 7th, 2018
NI KUFUATIA KUKITHIRI KWA MALALAMIKO YA WANANCHI KUHUSIANA NA TAKA ZILIZORUNDIKANA MITAANI.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh.Daniel Chongolo ametoa siku saba kwa wakandarasi wa huduma ya kuzoa taka pamoja na Manispaa kuhakikisha wanaboresha utoaji wa huduma hiyo kwenye mitaa husika ili kuondokana na kero inayowasumbua wananchi ya mrundikano wa matakataka.
Ametoa agizo hilo leo alipokuwa  katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijitonyama uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi  Kijitonyama kisiwani  kwa lengo la kusikiliza kero zao na kuzipatia majibu.
Amesema iwapo wananchi wanachangia fedha zao kwa ajili ya huduma hiyo, nilazima waipate, kwani kukithiri kwa  matakataka mitaani kwaweza kuleta magonjwa ya mlipuko yanayotokana na uchafu.
"Natoa agizo, kufika siku ya Jumanne kuanzia leo, kuwe na mwelekeo madhubuti wa kutoa taka kwenye Kata na Mitaa yetu" Ameagiza Chongolo.
Akitoa ufafanuzi wa swala hilo, Ndg Peter Abilu ambaye pia ni Afisa Usafishaji wa Manispaa hiyo amesema, kwa sasa Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Maafisa watendaji wa Kata na Mitaa, pamoja na Wakandarasi wa kuzoa taka tumeandaa mpango mkakati utakaoondoa kero hiyo na mazingira kubaki masafi.
Awali akitoa taarifa ya Kata ya Kijitonyama kwa Mkuu huyo wa Wilaya,  Mtendaji wa Kata hiyo Bi.Elizabeth Minga amesema Kata yake inajumla ya Mitaa Nane, shule za Msingi 7, Sekondari 4, vituo vya polisi 3, Zahanati 2, Masoko 3, Hotel 18, Nyumba za kulala wageni 31, na Bar 50.
Aidha ameainisha  changamoto kubwa zinazowakabili katika Kata hiyo kuwa ni wananchi kujimilikisha maeneo ya wazi, ujenzi juu ya mifereji na pembezoni mwa kingo, na uthibiti wa taka ngumu.
Akipokea maagizo na maelekezo ya Mkuu wa Wilaya, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa,  Ndg Maduhu Kazi  ambaye pia ni Afisa Mipangomiji ameahidi kuyafanyia kazi maagizo na maelekezo  yote yaliyotolewa, ikiwa ni pamoja na kutatua kero zinazowakabili wananchi.
Hii ni ziara yake ya pili ambapo ametembelea na kukagua miradi inayotekelezwa katika kata ya Kijitonyama, na kufanya mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wananchi, wakuu wa idara na vitengo pamoja na  viongozi mbalimbali wa Kata na Taasisi za Serikali ambapo ziara yake ya kwanza ilifanyika katika kata ya Bunju.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.

0 comments:

Post a Comment

 
Top