Top ad

Top ad

WAKULIMA NA WAFUGAJI KOTE NCHINI WAMETAKIWA KUZINGATIA UBORA WA BIDHAA WANAZOZALISHA ILI KUENDANA NA UHITAJI HALISI WA SOKO

Posted On: October 16th, 2018
Ni agizo lake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Omari Mgumba alipokuwa kwenye maadhimisho ya siku ya chakula duniani yenye kaulimbiu isemayo "Dunia bila njaa 2030 inawezekana", yaliyoadhimishwa  kimkoa katika kituo cha kilimo  Malolo, Kata ya Mabwepande, Manispaa ya Kinondoni.
Amesema maadhimisho haya yanayoadhimishwa tarehe 16/10 ya kila mwaka ni maadhimisho yenye lengo la kuonesha umuhimu wa  kukabiliana na baa la njaa,  kwani kauli mbiu ya mwaka huu inasadifu hayo na inatakiwa kutekelezwa kwa wakulima wetu kufanya kilimo cha  uzalishaji unaozingatia mahitaji, upatikanaji na ubora wa bidhaa ili kukabiliana na changamoto ya Masoko.
"Tulime kwa kuzingatia mahitaji, ubora, na masoko, kwani ubora ndio utakaosababisha bidhaa zetu ziuzike kwa urahisi". Amesisitiza Naibu Waziri.
Aidha Naibu Waziri huyo pia amewataka wasindikaji wa vyakula kuanzisha chama kikuu cha ushirika kitakachowaweka pamoja na kuwawezesha kupata mikopo kutoka kwenye mabenki na kubadilishana uzoefu utakaowasaidia kuongeza tija katika uzalishaji.
Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri, Mratibu wa wa maadhimisho hayo kwa Manispaa ya kinondoni ambaye pia ni Mkuu wa idara ya Kilimo Ndg Salehe Hija amesema kwa sasa kituo kinafanya utafiti wa ipi mbegu bora itakayoongeza tija katika Kilimo na kusaidia kupata mazao yanayohitajika hasa kwa wateja.
Maadhimisho hayo yaliyoadhimishwa kimkoa katika Kata ya Mabwepande Manispaa ya Kinondoni na kushirikisha  wajasiriamali, wakulima na wasindikaji kutoka Halmashauri ya  Ubungo, Ilala, Kigamboni na Temeke, pia yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali, kadhalika na  wadau mbalimbali kama vile KOICA na  NMB.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.

0 comments:

Post a Comment

 
Top