KINONDONI YAADHIMISHA SIKU YA KICHAA CHA MBWA DUNIANI KWA KUTOA CHANJO KWA MBWA NA PAKA 1150 KATI YA 1588, WALIOTAMBULIWA.
Posted On: September 28th, 2018
Manispaa ya Kinondoni leo imeadhimisha siku ya kichaa cha Mbwa duniani, yenye kauli mbiu isemayo "Sambaza ujumbe, okoa maisha" kwa kutoa chanjo kwa mbwa na paka 1150, zoezi lililofanyika katika Mtaa wa Madale, Kata ya Wazo iliyopo Manispaa hiyo.
Akizungumnzia maadhimisho hayo ambayo huadhimishwa duniani tarehe 29/08 ya kila mwaka, kwa niaba ya Afisa Mifugo wa Manispaa ya Kinondoni, Dr. Ntanga amesema, Kinondoni imemudu kudhibiti kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa, kwani chanjo iliyokwishatolewa tangu mwezi wa saba mwaka huu, hadi sasa ni asilimia 70.
"Viko viwango vya Afya kutoka shirika la Afya duniani vinavyosadikiwa kwamba, chanjo ya ugonjwa ikifanyika kwa asilimia 70, inakuwa imemudu kwa kiasi kikubwa zuio la ugonjwa husika. Kwa sisi Kinondoni tangu mwezi wa saba mwaka huu, hadi sasa tumefanikiwa kutoa chanjo kwa mbwa na Paka 1150 kati ya 1588 waliotambuliwa" Amebainisha Dr.Ntanga.
Aidha Dr Ntanga pia ametahadharisha athari zinazopatikana kwa kung'atwa na mbwa mwenye kichaa kuwa ni kupelekea kifo endapo matibabu yatacheleweshwa, na kuwataka wananchi wakazi wa Kinondoni kuhakikisha wanazingatia sheria ndogo za ufugaji mijini kwa kuhakikisha wanawapeleka mbwa wao na paka kwenye chanjo.
Maadhimisho hayo yameenda sambamba na uoneshaji wa sinema kwa wanafunzi inayotoa elimu na uelewa wa namna thabiti ya kujikinga na athari za kichaa cha mbwa.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment