KUELEKEA KAMPENI YA UTOAJI KINGA TIBA ZA KICHOCHO NA MINYOO YA TUMBO KWA MKOA WA DAR ES SALAAM
Posted On: August 28th, 2018
KINONDONI YATOA MAFUNZO KWA WAALIMU WA AFYA MASHULENI, NA WATOA HUDUMA, YA JINSI YA KUENDESHA ZOEZI HILO SIKU YA ALHAMISI
Kinondoni kupitia idara ya Afya kitengo cha magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, kimeendesha mafunzo ya siku moja kwa waalimu wa masuala ya Afya mashuleni, pamoja na watoa huduma kutoka vituo vya afya na zahanati za Serikali, wa jinsi ya kugawa kinga tiba kwa magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo, kwa wanafunzi kuanzia umri wa miaka mitano(5) hadi kumi na nne(14), kampeni inayotarajiwa kufanyika siku ya Alhamis.
Akizungumzia dhumuni la mafunzo hayo, Msimamizi wa Kampeni ya magonjwa hayo kwa Manispaa ya Kinondoni Dr.Neema Mlole amesema, mafunzo haya yanalenga kuwaandaa,waalimu katika kufanikisha zoezi hilo, likienda sambamba na kuwafundisha vigezo vinavyotakiwa kuzingatiwa wakati wa utoaji wa kinga tiba hizo kwa wanafunzi, kadhalika na kuwapatia vifaa vikihusisha kipimo cha urefu, na dawa hizo kwa ajili ya utekelezaji.
Amesema kuelekea siku ya Alhamisi ya tarehe 30/08/2018, Kinondoni inatarajia kutoa aina mbili za kinga tiba ambazo ni Prazguantel kwa magonjwa ya kichocho na Albendazol kwa Minyoo ya tumbo kwa wanafunzi takribani 121,086 kutoka shule 157, za Manispaa.
"Kinga tiba zitakazotolewa ni mbili, ambazo ni albendazol kwa ajili ya minyoo, na Prazguantel kwa ajili ya kichocho. Katika dawa hizi kabla ya kumpatia mtoto vipo vigezo vinavyotakiwa kuzingatiwa ambavyo ni kwanza Mtoto awe amekula chakula na kushiba, na pia apimwe urefu kwani Prazguantel kwa ajili ya kichocho idadi ya vidonge vyake huzingatia urefu." Amefafanua Dr.Neema.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa watoto hawa kupatiwa kinga tiba hizi ili waweze kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza, na kwamba dawa hizi hazina madhara yeyote kwa mwanadamu.
Mafunzo haya yaliyofanyika katika ukumbi wa Matakatifu Yosefu Manzese yamehusisha waalimu wa masuala Afya na watoa huduma vituo vya Serikali takriban 500, kwa lengo la kufanikisha kampeni hiyo ya utoaji wa kinga tiba siku ya Alhamisi tarehe 30/08/2018.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Uhusiano na habari.
Manispaa ya Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment