Mkuu wa Wilaya ya kinondoni Mh. Ali Hapi amezindua mpango wa Wilaya wa ukarabati barabara zilizoharibiwa na mvua zenye urefu wa Km 148.
Uzinduzi wa mpango huo uliofanyika leo ni kufuatia uharibifu mkubwa wa barabara uliojitokeza kwenye barabara za Kata katika kipindi cha msimu wa mvua uliopita na kusababisha adha kwa wananchi.
Akizindua mpango huo Hapi amesema upo mtandao wa barabara wenye jumla ya urefu wa Km 612.00 na kati ya hizo km 539.85 ndizo zinahudumiwa na Manispaa.
Amesema upo mpango wa uboreshaji wa jiji la Dar es Salaam unaoendelea kwa barabara ya Sokoni Makumbusho, MMK Nzasa, barabara ya viwandani na Tanesco soko la Samaki ambapo kwa ujumla wake zinaurefu wa Km 6.86 .
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amewapongeza wadau mbalimbali waliounga mkono Serikali katika kuhakikisha kuwa miundombinu ya kukarabati barabara inapatikana kwa wakati na katika ubora wa kufanya kazi.
Amezielekeza pongezi zake kwa Kampuni ya Total kwa kutoa mafuta ya dizel lita 10,000, na Grand Tech kwa mitambo ya Kazi.
Halikadhalika amewapongeza wananchi wa Kata za Manispaa ya Kinondoni pamoja na Taasisi kwa juhudi zao za kukarabati barabara korofi za Manispaa hiyo
0 comments:
Post a Comment