Top ad

Top ad





MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi leo ameendelea na ziara yake katika kata ya magomeni ambapo pia alishiriki kikao cha Kamati ya Maendeleo ya kata (WADC na kufanya mkutano na wananchi eneo la Magomeni Suna.
Katika ziara yake, Hapi amewataka watendaji wa mitaa na maafisa kata katika Manispaa hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Hapi alitoa kauli hiyo leo wakati alipofanya ziara katika Kata ya Magomeni iliyopo katika Wilaya hiyo kusikiliza kero za wananchi na kuangalia utendaji wa viongozi katika kata.
Alisema kuna baadhi ya viongozi na watendaji wa kata wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea wakiamini hakuna mtu anayeweza kuwafuatilia.
"Napenda sana msemo ambao aliupenda sana kuutumia Rais wa awamu ya Pili Ally Hasan Mwinyi. Nao ni kuwa kila zama na kitabu chake.
Hivyo ninawaomba mtambue kuwa zama tulizopo sasa ni zama mpya na kitabu chake ni kipya."
alisema Hapi.
Aidha DC Hapi amewaagiza watendaji hao kuwa na tabia ya kuwatembelea wananchi na kuona wana changamoto gani na kuzitafutia ufumbuzi na kuacha tabia ya kukaa ofisini.
"Kazi ya kiongozi sio kukaa ofisini pekee, bali ni kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi ikiwemo kuwatembelea na kutatua changamoto zao. Nimepata taarifa kuwa baadhi hawafiki hata ofisini wiki mbili,tatu sasa tabia hiyo iwe mwisho."aliongeza.
Akiwa katika mtaa wa Suna Magomeni, wananchi wa eneo hilo walitoa malalamiko yao juu ya uwepo wa baa katika eneo la Magomeni Makuti ambayo imekuwa ikipiga mziki usiku kucha na kusababisha fujo na kero kwa wananchi.
Kwa kauli hiyo ilimfanya Hapi kutoa maagizo kwa Polisi na watendaji wa Wilaya hiyo kufuatilia baa hiyo na endapo kuna ukweli basi hatua zichukuliwe ikiwemo kufutiwa leseni.
Pia ameliagiza jeshi hilo kufuatilia nyumba ambayo imelalamikiwa kuwa imekuwa ikiuza pombe haramu ya gongo pamoja na kuuza bhangi jambo ambalo limekuwa kero na kutengeneza wezi katika eneo hilo.
"Nimeisikia kero ya nyumba hii naagiza polisi kuifuatilia kabla mimi sijaenda hapo muhusika wa nyumba akamatwe ahojiwe, na nyinyi wananchi muwape ushirikiano na polisi wafanye kazi yao kwa kufuata sheria," alisema.

0 comments:

Post a Comment

 
Top