Top ad

Top ad

ZOEZI LA UGAWAJI WA HATI ZA VIWANJA KWA WANANCHI WA NYAKASANGWE KUANZA RASMI

Posted On: June 17th, 2020

Zoezi hilo la ugawaji wa hati za viwanja kwa  wakaazi wa maeneo ya Nakasangwe ni kufuatia  ukamilishaji wa upimaji viwanja 9741vya wananchi hao walioendeleza maeneo kiholela hali iliyopelekea tatizo sugu la uvamizi.

Zoezi hilo limetangazwa rasmi  na  Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe Daniel Chongolo alipokuwa akiongea na wananchi wa Nakasangwe, katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo viwanja vya shule ya msingi Nakasangwe.

Amesema kwa kuwamilikisha Wananchi maeneo yao kisheria  kutapunguza na kumaliza kabisa migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiwakabili siku za nyuma.

"Ninafahamu Katika kata hizi za pembezoni hususani Mabwepande kumekuwa na watu wachache wanaojishughulisha na uvamizi wa maeneo na kuwauzia Wananchi hali inayopelekea migogoro, Nipende tuu kuwakumbusha kuwa magereza zetu nchini zinahitaji nguvu Kazi, serikali haitokubali kuwaacha watu Hawa waendelee kusababisha migogoro kwenye maeneo yetu."

Naye mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji  Manispaa ya Kinondoni Ndg. Maduhu Kazi amesema  ugawaji huo wa hati ni kufuatia utekelezaji wa  maagizo ya Serikali yanayozitaka Manispaa kupima meneo yote yalioendelezwa kiholela.

Amesema viwanja vilivyopimwa ni 9741 ambapo kulikuwa na makundi ya    wenye migogoro na wasio na migogoro na kuwataka wanachi kufahamu kuwa ugawaji wa hati unaoanza kesho utahusisha maeneo ambayo hayakuwa na changamoto za migogoro.

Katika hatua nyingine, Mhe.Chongolo ameagiza wataalamu wa Manispaa kuanza kupima mtaa wa Mbopo  uliopo Kata ya Mabwepande ndani ya siku 14, na kuwataarifu  wanachi  wanaosababisha migogoro kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Zoezi la upimaji wa viwanja ni endelevu na litafanyika kwa awamu likihusisha maeneo yote yaliyoendelezwa kiholela.

Imeandaliwa na

Kitengo Cha habari na uhusiano

Manispaa ya Kinondoni.

0 comments:

Post a Comment

 
Top