Top ad

Top ad

KINONDONI YAINGIA MKATABA NA KAMPUNI MBILI UJENZI WA BARABARA, BILIONI 34.2 KUTUMIKA.

Posted On: March 10th, 2020
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni leo imesaini mkataba na Kampuni mbili za China kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa barabara zenye urefu wa kilomita 12 ambapo jumla ya  kiasi cha Tsh. Bil. 34.2 zitatumika kwenye mradi huo.
Kampuni ambazo Manispaa ya Kinondoni imeingia mkataba wa ujenzi huo  mara baada ya kutangazwa tenda ni Stecol Corporation pamoja na China Ralway Seventh Group Limited.
Mkataba huo umesainiwa na Mstahiki Meya Mhe. Benjamini Sitta, na kushuhudiwa na Kaimu Mkurugenzi Dk. Patricia Henjewele pamoja na Kaimu  Mhandisi wa Manispaa Mkelewe Tungaraza.  

 
Akizungumza mara baada ya hafla ya utiwaji wa saini wa mkataba wa mradi huo, Meya Sitta amefafanua kuwa  ujenzi huo utahusisha  barabara ya Magomeni mapipa hadi urafiki ambayo inaurefu wa zaidi ya kilomita saba (7), Makumbusho, Mwanamboka, na barabara ya Muhimbili ambazo zinaurefu wa zaidi ya kilomita tano (5).
Aidha Meya Sitta ameeleza kuwa  ujenzi wa barabara ya Magomeni Mapipa na Urafiki inajengwa na Kampuni ya Stecol Corporation kwa gharama ya  Tsh. Bil. 18.7 huku barabara ya Makumbusho, Mwanamboka na Muhimbili ikijengwa na Kampuni ya China Ralway Seventh Group Limited kwa gaharama ya Tsh. Bil.15.5.
Mhe. Sitta amemshukuru Mkurugenzi Aron Kagurumjuli kwa kuhakikisha barabara hizo zinajengwa na kwamba maendeleo ambayo yanafanyika katika Manispaa hiyo yanatokana na juhudi kubwa ya utendaji kazi wake.
“ Nampongeza Mkurugenzi wetu, anafanya kazi kubwa leo hii tunakwenda kuleta  maendeleo makubwa ya barabara katika Manispaa yetu, hivyo mradi huu utakuwa sehemu ya kutatua changamoto zilizopo katika Halmashauri yetu” amesema Meya Sitta.
“ Leo ni siku ya kihistoria katika Manispaa yetu, tumesaini mikataba mikubwa miwili kutoka kampuni mbili tofauti , mikataba hii nisehemu kubwa ya mradi wa DMDP, ambao unakwenda kutatua changamoto ya barabara kwenye Halmashauri yetu , hivyo ninampongeza sana Mkurugenzi wetu Kagurumjuli” amesema Meya Sitta.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa DMDP ambaye pia ni  Kaimu Mhandisi wa Manispaa,  Mkelewe Tungaraza amesema kuwa mradi huo utaanza Aprili mwaka huu na unatarajiwa kukamilika kwa muda wa miezi 15.

Imeandaliwa na
 Kitengo Cha habari na Mahusiano
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

0 comments:

Post a Comment

 
Top