KINONDONI YAADHIMISHA SIKU YA WAZEE DUNIANI KWA KUTOA HUDUMA ZA UPIMAJI WA AFYA BILA MALIPO Posted On: October 1st, 2019 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeadhimisha siku ya wazee duniani iliyoambatana na kauli mbiu isemayo "Tuimarishe usawa kuelekea maisha ya uzeeni" kwa kutoa huduma za Upimaji afya kwa wazee zaidi ya 200. Maadhimisho hayo yamefanyika leo katika viwanja vya mwinjuma vilivyoko katika Kata ya Makumbusho ambapo mgeni rasmi alikuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mh.Benjamin Sitta. Katika kuadhimisha siku ya wazee, Meya Sitta amesema changamoto kubwa inayowakabili wazee ni changamoto ya afya, hivyo Manispaa imeamua kupima afya za wazee hao na kutoa ushauri wa masuala ya afya kwa wazee ili kuweza kuimarisha afya zao. Pia ameitaja mikakati iliyowekwa na Manispaa ya kinondoni katika kuimarisha afya za wazee kuwa ni pamoja na kuhakikisha wanapata kadi za msamaha wa matibabu zitakazowapa uhakika wa matibabu bure katika vituo vyote vya afya na zahanati zote za serikali. Naye Afisa ustawi wa jamii wa Manispaa hiyo amesema Manispaa katika kuhakikisha inawapatia wazee matibabu bure, Tayari imeshagawa vitambulisho 12,183 vya matibabu bure kwa wazee wa kuanzia umri wa miaka 60 na zoezi hili ni endelevu. Katika hatua nyingine mwakilishi wa wazee amebainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili kuwa ni pamoja na kukosa baadhi ya dawa katika baadhi ya vituo vya afya, uchache wa vituo vya kulelea wazee wenye mahitaji maalum, posho ya kujikimu ya kila mwezi na kutokuwepo kwa miradi ya wazee ili iweze kuwasaidia kiuchumi. Huduma za afya zilizotolewa katika maadhimisho hayo ni pamoja na kupima pressure, kisukari, macho, elimu ya lishe, pamoja na kuandikisha kadi za msamaha wa matibabu. Imetolewa na Kitengo cha Uhusiano Manispaa ya Kinondoni. KINONDONI YAADHIMISHA SIKU YA WAZEE DUNIANI KWA KUTOA HUDUMA ZA UPIMAJI WA AFYA BILA MALIPO Posted On: October 1st, 2019 Halmashauri ya... + Read more »
JAMII YATAKIWA KUJENGA MAZOEA YA KUCHANJA MBWA NA PAKA ILI KUWAKINGA DHIDI YA UGONJWA HATARI WA KICHAA CHA MBWA Posted On: September 28th, 2019 Wito huo umetolewa na Tabibu wa mifugo mkoa wa Dar es salaam Dr Senorina Mwingira katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kichaa cha Mbwa Duniani yanayofanyika kila Tar 28 Septemba ambayo kwa wilaya ya Kinondoni yamefanyika viwanja vya Mbezi Ndumbwi. Dr Senorina amesema Kichaa cha mbwa ni hatari sana kwa binaadamu na wanyama kwani hakina tiba zaidi ya kinga hivyo niwapongeza sana Kinondoni kwa hamasa yenu kuhamasisha wananchi kuchanja Mifugo yao kwani si tu mnailinda jamii bali mnalinda haki za wanyama hawa pia. Naye Afisa Mifugo toka wilaya ya Kinondoni Bi Bertilla Lyimo kwa niaba ya Mkuu wa idara ya Mifugo wa Manispaa hiyo amesema chanjo hiyo itakuwa endelevu na zoezi hilo litafanyika kata kwa kata hivyo amewasihi wanajamii ya Kinondoni kufanya mwendelezo wa chanjo hii kwa manufaa yao na wanyama wao. Aidha amebainisha kuwa, waathirika wakubwa wa athari za kichaa cha mbwa ni watoto chini ya miaka 15, hivyo jamii itakapochukua hatua stahiki itakuwa imewalinda wahanga hao ambao ni watoto. Katika hatua nyingine kabla ya maadhimisho hayo, Manispaa ya Kinondoni ilionesha onesho la sinema kwa wanafunzi zaidi ya 800 toka shule ya msingi Mbezi Ndumbwi linaoelezea madhara ya ugonjwa wa Kichaa cha mbwa kwa binaadamu, ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa wanafunzi hatua za kuchukua endapo itatokea akang'atwa na mbwa au paka ili asiweze kupata ugonjwa hatari wa kichaa Cha mbwa. Manispaa ya Kinondoni imelenga kuchanja mbwa takribani 1342 na paka 246 katika kata zote 20 na hii ni dhamira ya kuendana na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo "UGONJWA WA KICHAA CHA MBWA: CHANJA MIFUGO YAKO ILI KUTOKOMEZA UGONJWA HUU(RABIES VAAACCINATE TO ELIMINATE) Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Uhusiano Manispaa ya Kinondoni JAMII YATAKIWA KUJENGA MAZOEA YA KUCHANJA MBWA NA PAKA ILI KUWAKINGA DHIDI YA UGONJWA HATARI WA KICHAA CHA MBWA Posted On: September 28th... + Read more »
KINONDONI YAANZA RASMI MABORESHO YA UFUKWE COCOBEACH Posted On: September 17th, 2019 Manispaa ya Kinondoni imeanza rasmi utekelezaji wa maboresho ya fukwe wa Cocobeach kwa kuikabidhi kampuni ya Tanzania Building works shughuli hizo za uendelezaji kwa mujibu wa makubaliano na michoro iliyopitishwa kisheria kwa ajili ya utekelezaji, ili iweze kutumiwa na watanzania kwa makusudi tarajiwa pindi itakapokamilika. Akiongea mara baada ya kukabidhi fukwe hiyo kwa ajili ya maboresho Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Benjamin Sitta amesema, mradi wa Cocobeach ni mradi wa kimkakati hivyo Manispaa imefuata taratibu zote za kisheria hadi kufikia mchakato rasmi ambao umekabidhiwa kwa ajili ya utekelezaji. "Kwa dhati ya moyo wangu niishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais wetu Mhe. Dr.John Pombe Magufuli kwa kuwajali watanzania na kuwaboreshea maeneo ya kupumzika, lakini pia kutupatia fedha za kuendeleza fukwe hii ya Cocobeach ambayo ni mradi wa kimkakati ili Halmashauri pia ziweze kujiendesha katika baadhi ya mambo, hii ni fursa pekee kwa Manispaa yetu ya Kinondoni kuhakikisha tunamuunga mkono Mhe. Rais kwa utekelezaji kwa kiwango kilichokusudiwa." Amefafanua Meya Sitta. Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ndg Aron T Kagurumjuli amesema uendelezaji wa mradi huu wa kimkakati wa fukwe pamoja na miradi mingine katika Manispaa yake imefuata taratibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kumpatia mkandarasi mzawa jukumu hili, hali inayozingatia uzalendo na kuwataka watumiaji wa ufukwe huo kuwa sehemu ya uendelezaji kwa kuonesha ushirikiano pale inapopasa hasa uvumilivu katika kipindi hiki cha maboresho na kurejea pale itakapokamilika. Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Tanzania Building Works ndg Iqbal Noray ameishukuru Manispaa na Serikali kwa ujumla kwa kuwaamini na kuahidi kuikamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi kilichopangwa kwa weledi na ubora uliokusudiwa. Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Uhusiano Manispaa ya Kinondoni. KINONDONI YAANZA RASMI MABORESHO YA UFUKWE COCOBEACH Posted On: September 17th, 2019 Manispaa ya Kinondoni imeanza rasmi utekelezaji wa... + Read more »
PONGEZI ZATOLEWA KATIKA UJENZI WA JENGO JIPYA LA MAMA NA MTOTO MWANANYAMALA Posted On: September 14th, 2019 Pongezi hizo zimetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Daniel Chongolo alipozuru katika hospitali ya Mwananyamala kujiridhisha na hatua za ujenzi wa jengo jipya la mama na mtoto linalojengwa na chuo cha MUST Mbeya lililohusisha uwekaji wa CT-scan na X ray limekamilika kwa kiwango kilichokusudiwa. Amesema kuzuru kwake hapo ni katika kuhakikisha shughuli zinazotekelezwa na Serikali katika nyanja mbalimbali na kugusa wananchi zinakamilika kwa kusudi mahususi hasa ikizingatiwa yeye ndiye mwakilishi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwatumikia wananchi Wilayani kwake. "Hakika ninawapongeza sana kwa ujenzi wa jengo hili lenye kiwango mahususi uliohusisha mtazamo wa mbali ulio chanya katika uwekaji wa vifaa muhimu, haya ndiyo mambo Serikali yetu inayataka, kuwa na ubunifu kama huu wa uwekaji wa CT Scan na X-ray katika ujenzi kwani uhitaji wake ni wa muhimu sana, huo ni uthubutu wa hali ya juu" Ameongeza Mh Chongolo. Naye Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya hiyo Dr. Daniel Nkungu katika mazungumzo yake amemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa uzalendo alionao katika ufuatiliaji wa miradi ya Serikali kwani kwa kuzuru kwake katika jengo hilo kunaamsha hamasa si tu ya utendaji kazi, bali umakini katika kuhakikisha miradi ya serikali inakamilika kwa tija iliyokusudiwa. Imeandaliwa na kitengo cha Habari na Uhusiano Manispaa ya Kinondoni. PONGEZI ZATOLEWA KATIKA UJENZI WA JENGO JIPYA LA MAMA NA MTOTO MWANANYAMALA Posted On: September 14th, 2019 Pongezi hizo zimetolewa leo... + Read more »
KINONDONI KUENDELEZA KIWANJA NA.1024 MWENGE KIHUDUMA NA KIBIASHARA KWA KUJENGA KITUO CHA MABASI Posted On: September 11th, 2019 Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Daniel Chongolo alipokutana na wafanyabiashara wa eneo hilo la Mwenge na kuzungumza nao katika kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Manispaa. Amesema kwa kufanya hivyo ni kwenda sambamba na utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi inayosisitiza suala zima la uboreshaji wa miundombinu katika nyanja mbalimbali ikiwemo huduma za jamii kwa wamachinga na wafanyabiashara katika shughuli zao za kujipatia kipato na kukuza uchumi wao. "Sisi tunamuongozo unaoitwa ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwenye ilani hiyo inasema wazi kabisa kwa kipindi cha miaka mitano tunaweka mazingira rafiki kabisa kwa wafanyabiashara yakihusisha maeneo ya biashara, mtaji na uhakika wa eneo hivyo hatuna budi kuhakikisha hilo ambalo lipo ndani ya uwezo wetu linafanikiwa" Amefafanua Chongolo. Aidha amefafanua kuwa uendelezaji huo utahusisha ujenzi wa maduka ya kati ya kibiashara(min- supermarket), sehemu za mamalishe, maduka ya rejareja, maduka ya spea za magari, saluni, vituo vya tax na bajaji, migahawa, vyoo vya jumuiya pamoja na huduma nyingine. Kadhalika amewataka wakazi na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika eneo la kiwanja1024 kuwa sehemu ya uendelezaji huo kwa kutoa ushirikiano pale inapopasa ili kwa pamoja turahisishe maendeleo yenye tija kwa biashara zetu na Taifa kwa ujumla. Alipokuwa akiongea mfanyabiashara mmoja kwa niaba ya wengine ameonesha kuupokea mradi huo na kuahidi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha unafanikiwa kwa kiwango chenye tija na kilichokusudiwa, na kuiomba serikali iwafikirie pia mara baada ya kukamilika kwake wawe wakwanza kupatiwa maeneo kwa ajili ya kufanyia biashara. Imeandaliwa na Kitengo cha habari na uhusiano Manispaa ya Kinondoni KINONDONI KUENDELEZA KIWANJA NA.1024 MWENGE KIHUDUMA NA KIBIASHARA KWA KUJENGA KITUO CHA MABASI Posted On: September 11th, 2019 Hayo ya... + Read more »
KINONDONI YAPOKEA MSAADA WA SAMANI ZA SHULE KUTOKA KWA INTERNATIONAL SCHOOL OF TANGANYIKA Posted On: September 6th, 2019 Akipokea msaada huo kutoka kwa Mkurugenzi wa IST Dr. Mark Hardeman, Mstahiki Meya Manispaa ya Kinondoni Mhe.Benjamini Sita amesema samani hizi zimekuja wakati ambao Serikali yetu ya awamu ya tano inasisitiza ubora wa miundombinu ya elimu, inayoenda sambamba na ushirikiano wa kielimu baina ya shule na shule kwa lengo la kukuza ujuzi katika kufundisha. Amesema suala la elimu nchini Tanzania limechukua sura ya kipekee hali inayopelekea viongozi kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanaendana na sera ya elimu bora na kubainisha kuwa Kinondoni tayari wamejipanga vizuri katika kuhakikisha wanatekeleza upatikanaji wa elimu bora na sio bora elimu. "Katika kuhakikisha tunaendana na kasi ya Mhe. Rais tunatakiwa kuwa wabunifu kila iitwapo leo, leo hii tumepata samani kwa ajili ya shule zetu mbili za Mbweni Teta na Kigogo pamoja na vitabu zaidi ya boksi 44 na tumefanikiwa kupata vifaa hivi kwa kuwa na ushirikiano mzuri na wenzetu wa International School of Tanganyika, hata hivyo tunarajia kupokea vifaa vingi zaidi." Ameongeza Meya. Aidha Msitahiki Meya amesema kuwa upo mfumo mpya ambao anatarajia kuutambulisha hivi karibuni ambao utakuwa chachu ya mafanikio ya elimu kwa Manispaa yake ambacho kitaweza kuinufaisha Nchi kwa ujumla. Naye Dr. Mark Hardeman kutoka International School of Tanganyika amesema kuwa ushirikiano uliopo baina ya Taasisi yake na Manispaa ya Kinondoni ni wa kipekee sana na ameahidi kudumisha na kunufaisha sekta mbalimbali zilizopo na zitakazobuniwa wakati wowote. Kadhalika Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Kinondoni Mwl. Leonard Msigwa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ameishukuru Taasisi hiyo ya shule kwa kuonesha ushirikiano wenye manufaa zaidi tena kwa mda muafaka . Imeandaliwa na Kitengo Cha Uhusiano na Habari Manispaa ya Kinondoni. KINONDONI YAPOKEA MSAADA WA SAMANI ZA SHULE KUTOKA KWA INTERNATIONAL SCHOOL OF TANGANYIKA Posted On: September 6th, 2019 Akipokea msaad... + Read more »
ELIMU YATOLEWA KUHUSIANA NA MABORESHO YA BARABARA -CHINI YA DMDP, KATIKA MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA SHEKILANGO -BAMAGA Posted On: August 24th, 2019 Elimu hiyo imetolewa leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya ofisi ya Afisa mtendaji Sinza ukiwahusisha wananchi wa Sinza A, B, C, D na E ambao ndio walengwa mahususi wa mradi. Katika mkutano huo wa hadhara ilielezwa kuwa Lengo kuu ni kuutambulisha mradi na kutoa elimu na ushauri utakaoweka Mazingira rafiki yatakayowezesha utekelezwaji wake, kwa kuzingatia weledi, ufanisi na ubora uliokusudiwa. Akiambatana na timu ya wasimamizi wa mradi huo, Bi. Pendo Fred, ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kinondoni amesema, ni vema kuundwa kamati za watu watano kila mtaa kwa lengo la kutoa taarifa stahiki kuhusiana na mradi mzima ikihusisha faida zitakazopatikana wakati na baada ya mradi kukamilika, kwani hiyo ndiyo njia sahihi itakayomwezesha mwananchi yeyote kutoa ushirikiano pale inapobidi, na pia kujua nini wajibu wake na namna ya kutoa taarifa ikiwa kutakuwa na shida yoyote inayoweza kuzalishwa na mradi wakati wa utekelezaji. Kwa upande wake Diwani wa kata ya Sinza Mhe Godfrey Chikandamwali amewashukuru na kuwaahidi wasimamizi wa mradi huo kuendelea kuwaunga mkono kwa kuwa miradi yote ni kwa faida ya wananchi na kusema jukumu walilofuata katika mkutano huo ni jema. Mradi huo utahusisha barabara ya Shekilango mpaka Bamaga awamu ya saba kwa urefu wa km 3.7 kwa usimamizi wa kampuni ya China Road and Bridge Corporation ambao tayari ulishaanza kutekelezwa tangu July 2019, na utakamilika Octoba 2019. Imeandaliwa na Kitngo cha Habari na Uhusiano Manispaa ya Kinondoni. ELIMU YATOLEWA KUHUSIANA NA MABORESHO YA BARABARA -CHINI YA DMDP, KATIKA MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA SHEKILANGO -BAMAGA Posted On: Aug... + Read more »